Serikali ya kijeshi ya Burkina Faso Jumatatu ilisitisha matangazo France 24 nchini humo baada ya kituo hicho cha televisheni kurusha hewani mahojiano na mkuu wa tawi la Afrika Kaskazini la al Qaeda -AQIM.
Uhusiano kati ya Paris na Ouagadougou umezorota sana tangu jeshi la Burkina Faso kukamata madaraka katika mapinduzi ya Oktoba mwaka jana.
Mwezi Januari Burkina Faso iliipa Ufaransa mwezi mmoja kuondoa wanajeshi wake huku ikihitimisha makubaliano ya kijeshi ambayo yaliwaruhusu wanajeshi wa Ufaransa kupambana na waasi ikiwa ni pamoja na katika eneo lake.
France 24 mapema mwezi huu ilirusha hewani mahojiano na Yezid Mebarek anayejulikana pia kama Abu Ubaydah Yusuf al-Anabi ambaye alidai kuchukua jina la Emir wa Al Qaeda katika Islamic Maghreb mwaka 2020 baada ya uvamizi wa Ufaransa kumuua mtangulizi wake.
Kwa kumhoji mkuu wa AQIM France 24 si tu inakuwa kama msemaji wa magaidi hawa lakini kilicho kibaya sana, inatoa nafasi ya kuhalalisha vitendo vya kigaidi na matamshi ya chuki waziri wa mawasiliano wa Burkina Faso Jean-Emmanuel Ouedraogo alisema katika taarifa yake.