Iwapo mswada huo utapita katika Seneti, basi utapelekwa kwa baraza la wawakilishi ili kupigiwa kura, wakati wabunge wakijaribu kuupitisha kabla ya muda uliowekwa kisheria kuisha, ambao ni saa sita usiku, saa za Washington.
Kiongozi wa walio wengi katika Seneti, Chuck Schumer, alisema mswada huo utahakikisha kwendelea na viwango vya hivi sasa vya ufadhili, katika mashirika na idara zote za serikali.
Hadi tarehe tatu mwezi Disemba. Ufadhili huo pia utajumuisha matumizi ya dola bilioni 6.3, kusaidia kuwaleta wakimbizi wa Afghanistan, wanaohamia hapa Marekani, baada ya utawala wa Biden kumaliza vita vya mika 20 nchini humo, na kiasi kingine cha dola bilioni 28.6, kusaidia majimbo ya Mashariki na Kusini, nchini Marekani, ambayo yameathiriwa vimbunga, na yale ya Magharibi yaliyoathiriwa na mioto ya misituni.
"Pamoja na masuala mengi muhimu kushughulikia, jambo la mwisho ambalo Wamarekani wanahitaji hivi sasa ni kufungwa kwa serikali," Schumer alisema katika hotuba yake kwenye Baraza la Seneti jana Jumatano.
Lakini kiongozi wa Warepublikan katika Seneti Mitch McConnell alisema wao wataunga mkono tu hatua ambayo inahusu ufadhili wa shughuli za serikali katika mwaka mpya wa fedha unaoanza Ijumaa.