Polisi nchini Senegal wamewafyatulia gesi ya machozi waandamanaji mjini Dakar wanaopinga mabadiliko yaliyopendekezwa juu ya sheria ya uchaguzi ambayo wapinzani wanasema itafanya iwe rahisi kwa Rais kuchaguliwa tena.
Mashahidi wanasema waandamanaji walirusha mawe kwenye jengo la bunge wakati mabishano yalipoanza Alhamis.
Mwandishi wa Sauti ya Amerika mjini Dakar alisema Jumatano kuwa waandamanaji waliharibu basi moja karibu na Place de Independence, eneo kubwa katika mji mkuu. Anasema polisi wa kutuliza ghasia waliwatawanya waandamanaji kwa gesi ya machozi na anasema maafisa wa polisi wamesambazwa kote mjini humo.
Ripoti kutoka Senegal zinasema pia kulikuwa na maandamano katika kiunga cha Pikine mjini Dakar na mji wa kati wa Kaolack.
Bunge la taifa la Senegal linatarajiwa kupiga kura Alhamis juu ya sheria iliyopendekezwa na chama tawala ambayo itapunguza idadi ya kura zinazohitajika kwa mgombea kushinda ili kuepuka duru ya pili ya uchaguzi. Wapinzani wanasema mabadiliko yatampendelea Rais aliyeko madarakani, Abdoulaye Wade.
Sheria iliyopendekezwa pia itabudi nafasi mpya ya Makamu Rais, ambayo wapinzani wanaamini inaandaliwa kwa ajili ya mtoto wa kiume wa bwana Wade.
Ubalozi wa marekani mjini Dakar uliwaonya raia wa Marekani mjini humo kuhusu maandamano zaidi Alhamis. Ubalozi uliwataka raia wa Marekani kuepuka mikusanyiko, ukisema maandamano yanaweza kubadilika haraka na kuwa ghasia.