Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Mei 26, 2024 Local time: 11:41

Sanders hatimaye amuidhinisha Biden kama mgombea urais


Aliyekuwa Makamu wa Rais wa Marekani Joe Biden (Kushoto) na Seneta wa jimbo la Vermont, Bernie Sanders.
Aliyekuwa Makamu wa Rais wa Marekani Joe Biden (Kushoto) na Seneta wa jimbo la Vermont, Bernie Sanders.

Seneta wa jimbo la Vermont la Marekani, Bernie Sanders, Jumatatu alimuidhinisha aliyekuwa makam wa rais Joe Biden kuwa mgombea wa urais kwa chama cha Democratic.

Katika mawasiliano kupitia njia ya video iliyowaunganisha wawili hao, Sanders aliahidi kumsaidia Biden kushinda uchaguzi wa Novemba mwaka huu, akimtaja Trump kuwa mtu hatari zaidi katika historia ya hivi karibuni ya Marekani.

Sanders na Biden walikuabliana kuunda tume maalum zitakazofanya kazi kwa pamoja kuhusu maswala ya sera, jinsi ya kushughulikia maswala muhimu ya mabadiliko ya hali ya hewa, afya na uhamiaji, miongoni mwa mengine.

Sanders aliahidi kuleta Pamoja timu yake ya kampeni na kushirikiana na ya Biden katika kampeni kuelekea uchaguzi mkuu wa mwezi Novemba mwaka huu.

“Tunakuhitaji katika White House. Nitafanya kila niwezalo kuhakikisha kwamba hilo linafanikiwa, Joe,” Sanders alimwambia Biden katika video iliyowekwa kwenye wavuti wa Biden na kusambazwa kwa mitandao ya kijamii.

Seneta huyo alimkosoa Rais Trump kwa jinsi amesimamia janga la maambukizi ya virusi vya Corona, pamoja na kumtaja kuwa mbaguzi mkuu wa rangi miongoni mwa mengine, akisisitiza kwamba anastahili kuondolewa madarakani.

Hatua ya Sanders kumuunga mkono Biden ambaye amakuwa mshindani wake mkuu katika kinyang’anyiro cha tiketi ya chama cha democratic, ni muhimu sana wakati chama hicho kinatafuta kuunganisha wafuasi wake dhidi ya Rais Trump katika uchaguzi ujao.

Biden alimshukuru Sanders kwa kumuidhinisha, akisema anamhitaji sana sio kushinda kiti cha urais, lakini hata katika kuongoza Marekani.

"Nadhani hatua yako ya kuniidhinisha ina maana kubwa sana. Ina umuhimu mkubwa sana kwangu. nadhani kuna watu watashangaa kwamba baadhi ya sera zetu hazifanani lakini tunakubaliana katika mambo mengi sana. Nitakuhitaji sana sio tu kushinda uchaguzi bali pia kuongoza taifa,” alisema Biden katika mazungumzo yao.

Biden, akimtaja Sanders kuwa rafiki, alisema ana matarajio makubwa sana kufanya kazi na Sanders akiahidi kufanya kila awezalo kutimiza matarajio yao.

Hii ni mara ya pili kwa Bernie Sanders, kuwania tiketi ya chama cha democratic katika uchaguzi wa urais bila mafanikio.

Mwaka 2016, alishindwa na Bi Hillary Clinton.

Baada ya Sanders kumuidhinisha Biden, walishiriki mazungumzo wakiangazia jinsi rais Trump ameshughulikia janga la maambukizi ya virusi vya Corona, maswala ya uchumi, gharama ya juu ya masomo, miongoni mwa mengine.

Waliulizana maswali na kujibu, katika mazungumzo ya ziada yaliyoanza baada ya Biden kumuuliza Sanders kama ana swali lolote la kumuuliza.

Walizungumzia pia kiwango cha chini cha mshahara wanachostahili kulipwa wafanyakazi, Biden akikubali pendekezo la Sanders kuweka kiwango cha chini kuwa dola 15 kwa saa.

“Tumekuwa marafiki, tumekosa kukubaliana katika baadhi ya mambo, lakini tumekuwa marafiki,” alisema Biden.

“Najua wewe ni mtu utakayeongoza bila ubaguzi. Unataka kushirikisha kila mtu, hata wale wasiokubaliana na wewe,” aliongezea Sanders katika mazungumzo yao.

Sanders ambaye amekuja kufahamika na wengi kama mdemokrat anayegemea kwa sera za kisosialisti, alitangaza kujiondoa kwenye kinyang'anyiro cha kuwania tikiti ya chama hicho wiki iliyopita, lakini wakati huo hakutangaza moja kwa moja kama angemuunga mkono Biden.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG