Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Desemba 05, 2024 Local time: 09:56

Samaki kutoka China waathiri soko la ndani Kenya


Wavuvi wakiandaa nyavu zao kabla ya kwenda kuvua huko Mbita Magharibi mwa Kenya tarehe 21 Februari 2021. Picha na SIMON MAINA / AFP.
Wavuvi wakiandaa nyavu zao kabla ya kwenda kuvua huko Mbita Magharibi mwa Kenya tarehe 21 Februari 2021. Picha na SIMON MAINA / AFP.

Wavuvi na wafanya biashara nchini Kenya wameitaka serikali ya rais William Ruto kukomesha uingizaji wa samaki kutoka China, ili kulinda ajira na sekta ya uvuvi nchini humo.

Wakizungumza na Sauti ya Amerika kwa njia ya simu, baadhi ya wavuvi na wafanyabiashara wa samaki wa Kisumu na maeneo mbalimbali ya jiji la Nairobi wamesema uingizaji wa samaki hususan aina ya Tilapia unawaathiri sana kiuchumi na kudhoofisha ushindani wa kibiashara wa ndani.

Wavuvi hao ambao huvua samaki kutoka Ziwa Victoria na kuwauza kwa bei ya jumla katika soko la samaki lililopo katika ufukwe wa Dunga huko Kisumu, wamesema samaki wanaotoka China wamejaa katika masoko ya miji hiyo na kuuzwa kwa bei ya chini zaidi ikilinganishwa na bei ya wavuvi wa ndani.

Misodhi Maurise, mvuvi wa miaka mingi katika ziwa Victoria, amesema uingizaji wa samaki umeathiri ajira na vipato vyao na kusababishia hali ngumu ya maisha.

“Siku hizi hatupati wateja wanaotaka kununua samaki katika soko letu kwa sababu samaki wapo kila mahali mjini” na kuongeza kuwa “ wateja hawawezi kutufuata sisi kwa sababu samaki kutoka china wanauzwa kwa bei nafuu”

Mvuvi mwingine Fredirick Odany, amesema kuzorota kwa biashara ya ndani ya samaki kunawapa changamoto katika kukidhi mahitaji ya familia zao kuanzia kodi za nyumba, ada za shule na mahitaji mengine muhimu kama chakula.

Muuza samaki katika soko la samaki huko Kisumu Kenya. Picha na Yasuyoshi CHIBA / AFP.
Muuza samaki katika soko la samaki huko Kisumu Kenya. Picha na Yasuyoshi CHIBA / AFP.

Wavuvi hao wamesema samaki kutoka China wanauzwa kwa bei ya chini, zaidi ya nusu ya bei ya samaki wanaouzwa katika soko la ndani na kuwafanya washindwe kufanya ushindani wa bei kwa sababu ya kupanda kwa gharama za vifaa vya uvuvi kama vile nyavu na vitanzi.

Wamesema samaki aina ya Tilapia wamekuwa wakiwaletea kipato kibubwa wavuvi na wafanyabiashara wa samaki wa Kenya kutokana na soko kubwa na kupendwa kwa samaki hao nchini humo.

“Ziwa victoria lina samaki wengi, serikali lazima isimamishe uingizaji wa samaki kutoka China” amesema Maurise

Ema Gladys Akinyi, mwanamke mfanyabiashara wa samaki anayenunua samaki kutoka kwa wavuvi wa ziwa Victoria na kusambaza katika miji ya Kisumu, Mombasa, Kakamega Eldoret na maeneo mbalimbali katika jiji la Nairobi, amesema soko la Tilapia limeathirika zaidi.

Na kutoa mfano “Tilapia ambao huingizwa kwa kiasi kikubwa kutoka China, huuzwa kwa kilo shilling 200 wakati katika soko la wenyeji mara nyingi tilapia huuzwa shillingi 300”

Wiki hii Mbunge wa Alego Usonga, Sam Atandi amewasilisha barua kwa spika wa bunge la Kenya Moses Wetangula, akitaka kuwasilisha mswaada wa kufanyia marekebisho sheria ya kodi ambayo itaweka ushuru wa forodha wa kiwango cha asilimia 20 kwa samaki wanaoagizwa nchini kutoka nje ya nchi hususani China .

-Imetayarishwa na Mariam Mniga, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG