Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Machi 16, 2025 Local time: 19:41

Rwanda yakubaliana na pendekezo kuhusu mkutano wa kujadili mzozo wa DRC


Rais Paul Kagame wa Rwanda, Joao Loourenco wa Angola na Felix Tshisekedi wa DRC. Picha ya AFP
Rais Paul Kagame wa Rwanda, Joao Loourenco wa Angola na Felix Tshisekedi wa DRC. Picha ya AFP

Rwanda Jumapili imekubaliana na pendekezo la kufanyika kwa mkutano utakaosimamiwa na SADC na Jumuia ya Afrika Mashariki kujadili mzozo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, huku Tanzania ikitangaza pia kwamba wanajeshi wake wawili waliuawa katika mapigano ya hivi karibuni.

Waasi wa M23 waliuteka mji wa Goma wiki iliyopita na kutishia kusonga mbele hadi mji mkuu wa Kinshasa.

Jumuia ya nchi za kusini mwa Afrika (SADC) siku ya Ijumaa ilitoa wito wa kufanyika kwa mkutano utakaosimamiwa na SADC na Jumuia ya Afrika Mashariki “kuamua juu ya suluhu la hali ya usalama nchini DRC”.

Wizara ya mambo ya nje ya Rwanda “imekubaliana na pendekezo hilo” na kuongeza katika taarifa kwamba “imekuwa ikiunga mkono kila mara suluhisho la kisiasa kwa mzozo unaoendelea huko DRC”.

Rais wa Rwanda Paul Kagame hakuhudhuria mkutano wa dharura wa SADC, lakini Rais wa DRC Felix Tshisekedi alihudhuria kwa njia ya mtandao. Rwanda sio mwanachama wa SADC.

Mkutano wa SADC uliitishwa baada ya wanajeshi wa Afrika Kusini na Malawi kuuawa katika mapigano karibu na Goma, ambako walikuwa wanahudumu katika kikosi cha nchi wanachama wa SADC (SAMIDRC). Kikosi hicho kilikuwa na jukumu la kuisaidia DRC kupata amani na usalama wa kudumu.

Jumapili, Tanzania ilitangaza kwamba wanajeshi wake wawili katika kikosi cha SAMIDRC waliuawa pia katika mapigano ya hivi karibuni. Msemaji wa jeshi Gaudentius Ilonda alisema wanajeshi wengine wanne walijeruhiwa na wanapewa matibabu huko Goma.

Wanajeshi 13 wa Afrika Kusini, raia watatu wa Malawi na mmoja wa Uruguay waliokuwa wanahudumu katika kikosi cha MONUSCO na SAMIDRC waliuawa pia katika mapigano ya DRC.

Forum

XS
SM
MD
LG