Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Oktoba 06, 2024 Local time: 13:14

Rwanda: Wanaharakati wataka uchunguzi wa kina kufuatia kifo cha Mihigo


Aliyekuwa mwanamziki wa Rwanda Marehemu Kizito Mihigo.
Aliyekuwa mwanamziki wa Rwanda Marehemu Kizito Mihigo.

Mashirika ya kutetea haki za kibinadamu yanataka serikali ya Rwanda kuruhusu uchunguzi huru na wa kina kuhusiana na kifo cha mwanamziki maarufu wa nyimbo za injili na maridhiano nchini humo, Kizito Mihigo. 

Polisi wa Rwanda wanasema Mihigo alijitoa uhai akiwa katika kizuizi cha polisi cha Ramera.

Katika taarifa, polisi walisema Mihigo mwenye umri wa miaka 39, alipatikana amejinyonga kwa kutumia shuka la kujifunika Jumatatu asubuhi.

Alikuwa amezuiliwa katika kituo cha polisi tangu wiki iliyopita baada ya kukamatwa wilayani Nyaruguru.

Taarifa ya polisi inasema Mihigo alikuwa anazuiliwa kwa kujaribu kuvuka mpaka kuingia Burundi kinyume cha sheria na maafisa wanaamini kwamba alikuwa anaenda kujiunga na kundi la waasi kupiga vita serikali ya rais Paul Kagame.

Mpaka kati ya Rwanda na Burundi una idadi kubwa ya wanajeshi wanaoshika doria kila siku tangu Rwanda ilipoanza kuripoti mashambulizi kutoka kwa waasi miaka miwili iliyopita.

Kulingana na mwandishi wa habari nchini Rwanda, Bryson Bichwa polisi wanafanya uchunguzi huku raia nchini humo wakiwa na mashaka kuhusu kifo hicho.

“Polisi wanasema kwamba Mihigo amejinyonga. Alikuwa anazuiliwa pekee yake katika chumba maalum. Amepatikana saa kumi na moja asubuhi akiwa amekufa kwa kujinyonga akitumia shuka la kujifunika, mwili wake ukinging’inia kwa dirisha,” alisema Bichwa katika mahojiano na VOA.

Mkurugenzi wa shirika la human rights watch Afrika ya kati Lewis Mudge amesema kuna maswali mengi kuhusiana na kifo cha Mihigo.

“Kifo cha Kizito Mihigo akiwa kizuizini kinazua maswali mengi sana yanayohitaji kuchunguzwa kabisa. Mara nyingi watu wanaotuhumiwa kwa makossa ya kukosoa serikali, hupatikana wamekufa katika mazingira yenye utata”, amesema Lewis.

Katika taarifa, shirika la Amnesty international limesema limeshtushwa sana na tukio hilo.

“mamlaka nchini Rwanda inastahili kuanzisha uchunguzi huru haraka iwezekanavyo kuhusu kifo cha Mihigo, kueleza kama kilitokana na ajali, kifo cha kawaida, kuuawa ama kujiua.”.Inasema ripoti ya Shirika hilo.

Marehemu Kizito Mihigo
Marehemu Kizito Mihigo

Mihigo ni miongoni mwa watu 2140 wakiwemo viongozi wa juu wa upinzani, walioachiliwa huru kutoka gerezani mwaka 2018, kufuatia msamaha wa rais Paul Kagame.

Wakati huo, Mihigo alikuwa amezuiliwa kwa makosa ya kupanga njama ya kumuua au kumuumiza rais Paul Kagame na viongozi wengine nchini humo.

Alikamatwa mwaka 2014 baada ya kutoa wimbo uliokosoa maafisa walio madarakani. Wimbo huo ulifungiwa na mamlaka Rwanda mda mfupi baada ya kutolewa.

Alianza kuimba akiwa na umri wa miaka 9, akiimba nyimbo za kanisa na za kuhimiza amani na maridhiano.

Alipoteza wazazi wote katika mauaji ya kimbari yam waka 1994.

Alitorokea Burundi alipokutana na watu wa familia yake walionusurika mauaji hayo.

Anaripotiwa kujaribu kujiunga na kundi la Rwandan patriotic army - RPA kwa nia ya kulipiza kisasi kwa niaba ya familia yake, kabla ya kurejea Rwanda mwaka 1994.

Baada ya kumaliza masomo ya shule ya upili, alijiunga katika chuo cha kikatoliki akitaka kuwa kuhani na kwa kutumia muziki, alitangaza kuwasamehe walioua baba yake.

Tamasha zake za muziki wa injili na maridhiano, zimekuwa zikiwavutia watu wengi mjini Kigali, hasa nyumbani alikozaliwa Kibeho.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG