Mahakama ya juu ya Rwanda imefungua njia kwa rais Paul Kagame kugombea wadhifa huo kwa muhula wa tatu wa kipindi cha miaka saba baada ya muda wake wa uongozi kumalizika mwaka wa 2017.
Mahakama hiyo imetoa uamuzi huo hivi leo kwamba kurekebisha katiba na kuondoa kipengele cha rais kuhudumu kwa mihula miwili ni halali, mradi utaratibu unaheshimu sheria. Chama cha upinzani cha Green Party kiliwasilisha changamoto mahakamani kuzuia mabadiliko yaliyopendekezwa, baada ya bunge la Rwanda kupitisha mswada mwezi Julai wa kuunga mkono muhula mwingine kwa rais Kagame.
Hata hivyo wapiga kura wanatarajiwa kutoa usemi wao kupitia kura ya maoni. Kagame ndiye rais wa karibuni miongoni mwa wengine wa Afrika ambao wameonyesha nia yao ya kuendelea kubakia madarakani.