Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Septemba 30, 2023 Local time: 22:37

Rwanda na Russia zatuma wanajeshi Afrika ya kati baada ya jaribio la mapinduzi


wanajeshi wa Cameroon walio Afrika ya kati

Serikali ya Rwanda imetuma wanajeshi wake Afrika ya kati kwa ajili ya kuimarisha ulinzi, baada ya kikosi chake cha kulinda amani kushambuliwa na waasi wanaoripotiwa kusonga karibu na mji mkuu wa Bangui.

Serikali za Rwanda na Afrika ya kati, zimemshutumu rais wa zamani Francois Bozize kwa kuunga mkono waasi hao wanaopanga kupindua serikali.

Bozize amekana madai hayo dhidi yake.

Wanajeshi wa kulinda amani wa umoja wa mataifa wamesema kwamba waasi hao wameshindwa nguvu na kuzuiwa kuingia mji mkuu wa Bangui.

Bozize amezuiliwa kugombea urais utakaofanyika Jumapili.

Kulingana na msemaji wa serikali ya Afrika ya kati Ange Mazime Kazagui, Russia imetuma mamia ya wanajeshi na silaha nzito nzito Afrika ya kati kwa ajili ya kupigana na waasi hao.

Kazangui amesema kwamba wanajeshi wa Russia waliombwa kuingia nchini humo kama sehemu ya mkataba wa ushirikiano.

Rwanda haijatoa idadi ya wanajeshi ambao imetuma Afrika ya kati, lakini imesisitiza kwamba wanajeshi wake wameenda nchini humo chini ya makubaliano ya ushirikiano na Afrika ya kati.

Karibu wanajeshi wa Rwanda 750 na maafisa wa polisi, wamekuwa wakishika doria Afrika ya kati, kama kikosi cha kulinda amani cha umoja wa mataifa – MINUSCA.

Rais Faustin Archange Touadera, amesisitiza kwamba uchaguzi wa Jumapili utafanyika kama ulivyopangwa na kwamba raia wa nchi hiyo wasiogope kupiga kura kwa sababu usalama umeimarishwa.

Vyama vya upinzani kikiwemo chake Bozize, vinataka uchaguzi huo kuahirishwa.

Waasi wameteka miji kadhaa iliyo karibu na mji mkuu na mapigano makali kushuhudiwa kati ya waasi hao na wanajeshi wa serikali.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG