Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Julai 20, 2024 Local time: 06:07

Polisi Rwanda yaokoa raia 13 wa Burundi


Wakimbizi wa Burundi waliokimbia uvunjifu wa amani
Wakimbizi wa Burundi waliokimbia uvunjifu wa amani

Polisi nchini Rwanda inawashikilia watu 13 wanaoshukiwa kuwa walikuwa wakisafirishwa kinyume cha sheria kwenda bara la Asia.

Polisi wanasema watu hao ni raia wa Burundi ambao walikuwa njiani kwenda Kenya kupitia Uganda kwa ajili ya kusafirishwa kwenda Asia chini ya mtandao wa biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu.

Mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili VOA amesema hii si mara ya kwanza polisi nchini Rwanda kuwakamata raia wa Burundi ambao hupitia nchini Rwanda hadi Kenya ambapo yasemekana wanawakuta wasafirishaji haramu ambao huwachukua hadi nchi za Uarabuni na Asia.

Amesema waliokamatwa ni watu 12 na mtu mwingine ambaye ni raia wa Burundi anadaiwa kuhusika katika kuwapeleka watu hao Kenya ambako wangekutana na watu 2 waliokuwa wamejiandaa kuwasafirisha. Hata hivyo mpango huo uliharibika kabla ya kutekelezwa.

Baadhi ya wale waliokuwa wakipelekwa mmoja wao alijitambulisha kwa jina la Georgette kwamba yeye na wenzie hawakujua wanapelekwa wapi isipokuwa matumaini yao ilikuwa watapata ajira huko waendapo.

Msemaji msaidizi wa jeshi la polisi nchini Rwanda, Lynder Nakuranga amesema tatizo la biashara hiyo haramu halipo kwa kiasi kikubwa nchini Rwanda lakini bado jeshi hilo limejipanga vya kutosha kuhakikisha watu wanaojihusisha na vitendo hivyo wanakamatwa.

Polisi wamesema wengi ya washukiwa wanapokamatwa hawakubali kuhusika kwao kwenye visa hivyo licha ya kuwepo na ushahidi wa kujihusisha na vitendo hivyo vya uvunjaji wa sheria.

Kwa sasa raia hao wa Burundi ambao wengi wao wameshtushwa na kile ambacho kingewapata wanasubiri kurejeshwa nchini kwao wakati mshukiwa akisubiri kupelekwa mahakamani.

Imeandaliwa na Mwandishi wa idhaa ya Kiswahili VOA Sylivanus Karemera, Rwanda.

XS
SM
MD
LG