Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Desemba 09, 2023 Local time: 11:53

Ruto ateua baraza la mawaziri, wakuu wa polisi na jinai wang’atuka


Rais wa Kenya Dkt William Ruto akiwasalimu watu waliojitokeza katika uwanja wa michezo wa Kasarani jiji Nairobi wakati wa kuapishwa kwake September 13 2022
Rais wa Kenya Dkt William Ruto akiwasalimu watu waliojitokeza katika uwanja wa michezo wa Kasarani jiji Nairobi wakati wa kuapishwa kwake September 13 2022

Rais wa Kenya Dkt. William Ruto amewateua mawaziri 21 kwenye baraza lake la mawaziri ambao wataongoza utawala wake katika miaka mitano ijayo ya uongozi wake.

Ruto amemteua aliyekuwa makamu wa rais Musalia Mudavadi kuwa Mkuu wa Mawaziri, na gavana wa zamani wa Benki Kuu ya Kenya Profesa Njuguna Ndung'u kuwa Waziri wa Fedha.

Katika baraza hilo la mawaziri, lililo na wanawake saba, Ruto pia amemteua Profesa Kithure Kindiki ambaye alikuwa mmoja wa mawakili wake kwenye kesi dhidi yake katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ya ICC kuwa Waziri wa Usalama.

Prof Kindiki amekuwa seneta wa kaunti ya Tharaka Nithi kwa muda wa miaka 10 kati ya mwaka 2013 na 2023.

Rais Ruto ametangaza baraza la mawaziri muda mfupi baada ya kuongoza mkutano kamili wa baraza la mawaziri waliohudumu katika utawala wa rais wa zamani Uhuru Kenyatta, katika ikulu ya Nairobi.

Kikao hicho kiliangazia uchumi wa Kenya, kutathmini ya hali ya ukame nchini humo na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola katika nchi jirani ya Uganda.

Karibu nusu ya baraza la mawaziri ni wanawake

Baraza hilo la mawaziri limetangazwa wiki mbili baada ya kuapishwa kuwa rais wa Jamhuri ya Kenya

Wanawake 7 wameteuliwa katika nafasi za uwaziri. wanawake 3 wameteuliwa katika nafasi zinazohusiana na baraza la mawaziri kama washauri na katibu. Kwa jumla, wanawake 10 wameteuliwa katika baraza hilo la mawaziri lakini 7 ndio mawaziri kamili.

Alikuwa ameahidi kwamba nusu ya baraza hilo la mawaziri (21) watakuwa wanawake.

Wanawake walioteuliwa katika baraza la mawaziri

  • Alice Wahome - Maji
  • Aisha Jumwa - Huduma ya Umma
  • Rebecca Miano – Jumuiya ya Afrika Mashariki
  • Soipan Tuya – Mazingira
  • Susan Wafula – Afya
  • Peninah Malonza – Utalii
  • Florence Bore – Kazi
  • Monica Juma – Mshauri wa Usalama wa Taifa
  • Harriet Chiggai – Mshauri kuhusu Haki za Wanawake
  • Mercy Wanjau – katibu wa baraza la mawaziri

Aliyekuwa naibu wa waziri mkuu, Musalia Mudavadi, kupitia amri ya kiutendaji, ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mawaziri.

Mudavadi atakuwa na jukumu la kuongoza na kuratibu utekelezaji wa miradi ya serikali na kusimamia ajenda za sheria katika wizara zote.

Mudavadi ana umri wa miaka 62. Ndiye mwanasiasa mwenye uzoefu wa muda mrefu katika utawala wa Rais William Ruto. Mudavadi aliingia katika siasa akiwa na umri wa miaka 29.

Aliwahi kugombea urais. Amekuwa naibu wa waziri mkuu, waziri wa fedha, waziri wa serikali za mitaa na naibu wa rais katika utawala wa rais wa pili wa Kenya hayati Daniel Arap Moi.

Mkuu wa Polisi na mkuu wa upelelezi wa Jinai wang’atuka

Rais Ruto vile vile ametangaza kujiuzulu kwa hiari kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai George Kinoti na Inspekta Mkuu wa Polisi Hillary Mutyambai.

Ruto amesema kwamba Mutyambai amejiuzulu kutokana na sababu za kiafya. Alilazwa hospitali mwezi Agosti kabla ya kuondoka.

Alikuwa amebakisha muda wa miezi sita kumaliza muda wake ofisini.

Mutyambai na George Kinoti, wameshutumiwa sana na watu walio karibu na Ruto kwa kuwakandamiza kwa manufaa ya wapinzani wao wakati wa kampeni kuelekea uchaguzi mkuu.

Kinoti vile vile alijikuta katika majibizano na tume ya uchaguzi kuhusu usimamizi wa uchaguzi huo siku chache kabla ya uchaguzi.

Aliyekuwa gavana wa benki kuu ateuliwa kuwa waziri wa fedha

Gavana wa zamani wa Benki Kuu ya Kenya Profesa Njuguna Ndung'u ameteuliwa kuwa Waziri wa Fedha. Bw Ndung’u alihudumu kama gavana wa benki hiyo kwa mihula miwili ya miaka minne kila mmoja kati ya Machi 2007 hadi Machi 2015, katika utawala wa Mwai Kibaki na Uhuru Kenyatta.

Mbunge wa Garissa Mjini na Kiongozi wa zamani wa Shughuli za serikali katika bunge la Taifa, Aden Duale ameteuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi huku Seneta wa jimbo la Elgeyo Marakwet na Kiongozi wa zamani wa Shughuli za serikali katika baraza la Seneti Kipchumba Murkomen ameteuliwa kuwa Waziri wa Barabara na Uchukuzi.

Aliyekuwa gavana wa jimbo la Machakos, Dkt Alfred Mutua ameteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje.

Kabla ya kuwa gavana, Dkt Mutua alikuwa msemaji wa serikali wakati wa utawala wa aliyekuwa rais wa tatu wa Kenya hayati Mwai Kibaki.

Alisoma na kufundisha nje ya Kenya kabla ya kurudi Kenya.

Afisa Mratibu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Mbunge wa zamani wa Budalang’i Ababu Namwamba ameteuliwa kuwa Waziri wa Michezo.

Rebecca Miano ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya uzalishaji nishati nchini Kenya, KenGen, tangu mwaka 2017 na kuwa na tajriba ya takriban miaka 30 katika sekta ya nishati ameteuliwa kuwa Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, na Maeneo Kame.

Wengine walioteuliwa kuwa mawaziri

Moses Kuria ni Waziri wa Biashara, Susan Wafula, Afya, Eliud Owalo, ICT, Davis Chirchir, Kawi, Ezekiel Machogu, Elimu, Salim Mvurya, Madini, Florence Bore, Kazi, Simon Chelugui, Vyama vya Ushirika na Biashara ndogondogo, Penina Malonzo, Utalii, Zecharia Njeru, Ardhi, Mithika Linturi, Kilimo, Aisha Jumwa, Utumishi wa Umma, Alice Wahome, Maji na Soipan Tuya kuwa Waziri wa Mazingira na Misitu.

Pia, Ruto amemteua aliyekuwa Spika wa bunge la Taifa Justin Muturi kuwa Mwanasheria Mkuu, aliyekuwa Waziri wa Nishati Monica Juma kuwa Mshauri wake kuhusu masuala ya usalama, Mercy Wanjau kuwa Katibu wa Baraza la Mawaziri na wakili Harriet Chiggai kuwa Mshauri wake wa Masuala ya Wanawake.

Imetayarishwa na Kennedy Wandera, VOA, Nairobi

XS
SM
MD
LG