Afisa mwandamizi wa jeshi la wanamaji la Russia aliwaeleza wanahabari katika mkutano nao mjini Richards Bay, pwani ya mashariki mwa Afrika Kusini, kwamba nchi hiyo haina mpango wa kurusha kombora la Zircon wakati wa mazoezi ya siku kumi, Reuters iliripoti Jumatano.
Chombo kinacho beba silaha hiyo, Admiral Gorshkov, kiko katika maji ya Afrika Kusini, moja ya meli kadhaa za Russia zilizopelekwa kwenye zoezi la Mosi II.
Shirika la habari la Russia, TASS liliripoti mapema mwezi huu kwamba kombora la Zircon, ambalo Rais wa Russia, Vladimir Putin ameliita lisilo zuilika linaweza kutumika katika uzinduzi wa mafunzo wakati wa zoezi hilo.
Jambo hilo lilipingwa na chama kikuu cha upinzani cha Afrika Kusini cha Democratic Alliance pamoja na chama cha Wa-Ukraine wa Afrika Kusini.
Lakini hata hivyo Maafisa wa Afrika Kusini walikanusha ripoti hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari Jumatano, Kapteni Oleg Gladkiy, ambaye anaongoza kikosi cha Russia, amesema kombora la kasi kubwa halitatumika katika mazoezi hayo na hakuna cha kuficha, kwa mujibu wa wa Reuters.
Afrika Kusini imekosolewa vikali kwa kuendelea na mazoezi hayo, ambayo yanaambatana na kumbukumbu ya mwaka wa mmoja wa vita vya Ukraine vinavyoendelea.
Lakini serikali ya Afrika Kusini, ambayo haijaegemea upande wowote katika mzozo huo, imetetea haki yake ya kufanya mazoezi na marafiki.
Chama tawala cha African National Congress kina uhusiano wa muda mrefu na Moscow, tangu siku ambazo Umoja wa Kisovieti uliunga mkono mapambano ya ANC dhidi ya utawala wa weupe walio wachache.