Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Oktoba 07, 2024 Local time: 23:29

Paul Rusesabagina kukaa rumande Rwanda kwa siku 30 zaidi


Paul Rusesabagina ambaye anakabiliwa na mashtaka 13 ikiwemo ya ugaidi, mauaji na uandikishaji wanajeshi watoto.
Paul Rusesabagina ambaye anakabiliwa na mashtaka 13 ikiwemo ya ugaidi, mauaji na uandikishaji wanajeshi watoto.

Mahakama ya Rwanda imeeleza kwamba makosa yanayomkabili Rusesabagina ya ugaida na mengineyo ni makubwa na kutokana na hilo ataendelea kubaki rumande kwa siku nyingine 30.

Mahakama ya Rwanda, Alhamisi imemnyima dhamana Paul Rusesabagina, ambaye hadithi yake wakati wa mauaji ya halaiki nchini humo, ilifanyiwa filamu ya Hotel Rwanda.

Mahakama imeeleza kwamba makosa yanayomkabili ya ugaidi na mengineyo ni makubwa, na kutokana na hilo ataendelea kukaa rumande kwa siku nyingine 30.

Rusesabagina, ambaye ni raia wa Ubelgiji amekuwa akimkosoa rais Paul Kagame, anakabiliwa na mashitaka 13 ikijumuisha kufadhili ugaidi, kushiriki katika mauaji, kuandikisha wanajeshi watoto, na kuunda kundi la uasi.

Kama atakutwa na hatia huenda atakabiliwa na kifungo cha miaka 25 gerezani. Haijulikani ni lini kesi yake itasikilizwa tena.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AP, Rusesabagina mwenye umri wa miaka 66, kwa mara ya kwanza ameelezea namna alivyopotea alipokuwa matembezini Dubai, na baadaye kuonekana akiwa amefungwa pingu nchini Rwanda.

Kwa mujibu wa familia yake, Rwanda ni nchi ambayo Rusesabagina asingerejea kwa hiyari yake mwenyewe.

Akiongea na gazeti la The New York Times, chini ya uangalizi wa maafisa wa serikali ya Rwanda, Rusesabagina amesema alidhani ndege binafsi aliyopanda Dubai, ilikuwa ikielekea Bujumbura, Burundi.

Akiwa huko alipanga kwenda kuzungumza katika makanisa baada ya kupata mwaliko wa mchungaji.

Badala yake, Rusesabagina, alivyoshuka tu kwenye ndege, alizungukwa na wanajeshi wa Rwanda, kwa mujibu wa ripoti hiyo.

Baada ya hapo alifungwa, na kuzibwa uso na kutojua kule alikokuwa.

Mahakama ya Rwanda, imeeleza Rusesabagina alikamatwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Rwanda, na kuzusha utata wa taarifa ya awali ya polisi kwamba alikamatwa kwa ushirikiano wa kimataifa.

XS
SM
MD
LG