Sunak, anaingia madarakani wakati Uingereza inakabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi huku mamilioni ya watu nchini Uingereza wanakabiliana na hali ngumu ya maisha kutokana na kuongezeka kwa bei ya bidhaa muhimu na nishati.
"Nitaangazia zaidi ukuaji wa kiuchumi katika ajenda kuu ya serikali. Hii inamaanisha kwamba itabidi hatua ngumu kuchukuliwa. Lakini mliniona wakati wa janga la Covid nikichukua kila hatuailikuwa kulinda watu na biashara zao kwa mikakati mbalimbali. Kuna kiwango cha juu kinachoweza kuchukuliwa. Nawaahidi kwamba nitachukua hatua kama hizo kutatua changamoto tunazokabiliana nazo kwa sasa," amesema Sunak.
Sunak mwenye umri wa miaka 42, amekutana na mfalme Charles wa III, aliyeidhinisha uteuzi wake, muda mfupi baada ya kupokea rasmi ombi la Liz Truss kujiuzulu.
Anakuwa waziri mkuu wa Uingereza mwenye umri wa chini zaidi katika kipindi cha zaidi ya miaka 200.
Kujenga uchumi, kuunganisha chama cha Conservative
Anatarajiwa kuanza kuunda baraza lake la mawaziri litakalofanya kazi kuhakikisha kwamba Uingereza inatoka kwenye mgogoro wa uchumi. Ana kazi pia ya kujaribu kukiunganisha chama cha Conservative ambacho kimegawanyika baada ya kujiuzulu kwa Truss na kilichoingia katika mgogoro mkubwa na kupelekea kujiuzulu kwa Boris Johnson.
"Serikali ninayoongoza haitawacha nyuma Watoto na wajukuu wenu wakiwa na madeni ya kulipa ambayo tulishindwa kulipa wenyewe. Nitafanya kazi kila siku kuhakikisha kwamba tunatimiza kwa niaba yenu. Serikali hii itafanya kazi kwa kuzingatia uadilifu, weledi na uajibikaji katika kila sehemu. Uaminifu unapatikana, na nitapata wako."
Akizungumza katika makao ya waziri mkuu mjini London, Sunak amesema kwamba Truss alifanya makosa katika baadhi ya maamuzi yake lakini akaahidi kurejesha udhibiti wa uchumi na Imani ya watu wa Uingereza.
Hotuba ya mwisho ya Liz Truss
Waziri mkuu anayeondoka Liz Truss, katika hotuba yake ya kuondoka ofisini, amesema kwamba Lengo kubwa la Uingereza linastahili kuwa nchi iliyostawi.
"Tunastahili kuchukua fursa ya uhuru wetu wa kuondoka Umoja wa Ulaya na kufanya vitu kwa njia tofauti. Hii ina maana kwamba tunastahili kuhakikisha kwamba watu wetu wanastahili kuwa huru na kuhakikisha kwamba taasisi zetu zina mamlaka ya kutosha. Ina maana ya kupunguza kodi ili watu kuwa na uwezi wa kuweka akiba zaidi ya mshahara wanaopata. Ina maanisha kuhakikisha kwamba kuna ukuaji ili kuwepo usalama wa ajira, malipo ya juu na nafasi nzuri kwa Watoto na wajukuu wetu," amesema Liz Truss.