Kremlin imesema kuwa viongozi wa Russia na Ufaransa wamekubaliana kuimarisha ushirikiano wa kijeshi na mkakati nchini Syria baada ya mashambulizi yaliotokea Paris na kupigwa bomu kwa ndege ya Russia.
Taarifa hiyo ya Kremlin inasema rais wa Russia Vladimir Putin na mwenzake wa Ufaransa Francois Hollande Jumanne wamekubaliana kwa njia ya simu kushirikiana katika kukabiliana na vikundi vya kigaidi nchini Syria.
Taarifa hiyo inafuatia nyingine kutoka kwa Putin akiamuru jeshi la wanamaji la Russia lililoko kwenye bahari ya Mediterranean kuendeleza uhusiano wake na jeshi la wanamaji la ufaransa lililoko kwenye eneo hilo dhidi ya kundi la Islamic State.
Rais wa Russia aliasema hayo baada ya Hollande kusema kuwa meli ya kijeshi inayobeba ndege za kivita kwa jina Charles de Gaulle itapelekwa katika eneo la mashariki mwa Mediterranean. Rais Hollade atakutana na raisa Obama hapa Washington novemba 24 na siku mbili baadae aelekee Moscow kukutana na Putin ili kujadili vita dhidi ya kundi la Islamic State.