Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Aprili 22, 2025 Local time: 13:09

Rais wa zamani wa Mauritania akana mashtaka ya ufisadi dhidi yake


Rais wa zamani wa Mauritania Mohamed Ould Abdel Aziz
Rais wa zamani wa Mauritania Mohamed Ould Abdel Aziz

Rais wa zamani wa Mauritania Mohamed Ould Abdel Aziz Alhamisi alikanusha mashtaka ya ufisadi na kujitajirisha kwa njia haramu, katika kesi nadra ya ulaji rushwa dhidi ya rais wa zamani.

Aziz ambaye aliiongoza Mauritania kuanzia mwaka wa 2008 hadi 2019, alishtakiwa mwezi Januari mwaka huu pamoja na wengine 10, akituhumiwa kutumia vibaya mamlaka yake ili kujilimbikizia mali haramu.

Akiwa mahakamani mjini Nouakchott, Aziz alisema” Mashtaka haya hayana msingi na hamna ushahidi wowote kuyahusu.”

Aziz, mwenye umri wa miaka 66 na jenerali wa zamani wa jeshi, anakabiliwa na mashtaka ya kujitajirisha kwa njia haramu, kutumia vibaya madaraka, kushawishi biashara na utakatishaji wa fedha. Aliendelea kukana kufanya kosa lolote.

Watuhumiwa wenza ni pamoja na mawaziri wakuu wawili wa zamani, vile vile mawaziri wa zamani na wafanyabiashara.

“Mimi ni mwathirika wa njama ya wale niliowapinga,” Aziz alisema baada ya mahakama kumsomea mashtaka baada ya kesi kuahirishwa mara mbili.

Kama hapo awali, Aziz aliitaja katiba ya Mauritania, akisema inakataza hatua ya kumshtaki rais kwa vitendo alivyofanya akiwa madarakani.

XS
SM
MD
LG