Wanajeshi wa Tunisia walimzuia spika wa bunge kuingia katika jengo la bunge la nchi hiyo mapema Jumatatu, saa chache baada ya Rais Kais Saied kutangaza kuwa amemfukuza kazi Waziri Mkuu Hichem Mechichi na kusitisha bunge kwa siku 30.
Saied alisema alikuwa akifanya hivyo kwa kupambana na madhila ya kiuchumi ya nchi hiyo na mkwamo wa kisiasa na akaongeza kuwa katiba ya nchi hiyo ilimpa mamlaka hayo.
Rached Ghannouchi, spika wa bunge na mkuu wa chama cha Ennahdha, alikiita kitendo cha rais ni "mapinduzi" na akasema bunge litaendelea na kazi yake.
Vyama vingine viwili vikuu bungeni pia vilikiita kitendo hicho mapinduzi, ambapo rais alikanusha.
Tangazo la Saied lilipelekea umati wa waandamanaji katika barabara kwenye mji mkuu, Tunis, na sehemu nyingine kusherehekea.
Kulikuwa pia na waandamanaji nje ya jengo la bunge na baadhi ya mapigano kati ya makundi yanayopingana.