Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 19, 2024 Local time: 11:02

Rais wa Ghana na mawaziri wake wapunguza mishahara yao kwa asilimia 30.


Rais wa Ghana na mwenyekiti wa ECOWAS Nana Akufo-Addo akihudhuria mkutano wa pili wa dharura wa ECOWAS, kujadili mapinduzi ya kijeshi nchini Burkina Faso, mjini Accra, Februari 3, 2022. Picha ya Reuters.
Rais wa Ghana na mwenyekiti wa ECOWAS Nana Akufo-Addo akihudhuria mkutano wa pili wa dharura wa ECOWAS, kujadili mapinduzi ya kijeshi nchini Burkina Faso, mjini Accra, Februari 3, 2022. Picha ya Reuters.

Rais wa Ghana Nana-Akufo Addo na mawaziri wake wamepunguza mishahara yao kwa kiwango cha asilimia 30 kama hatua za kupunguza matumizi ya serikali, wakati nchi inakabiliwa na gharama kubwa za mafuta kutokana na mzozo wa Ukraine na kukwama kwa mswada wa sheria kuhusu kodi mpya.

Waziri wa fedha Ken Ofori-Atta ametangaza marufuku ya safari za nje kwa maafisa wa serikali, isipokuwa zile zenye umuhimu mkubwa, na ununuzi wa magari yanayoagizwa nje umesitishwa mara moja.

Amesema serikali inatarajia kuokoa karibu dola milioni 400 kupitia hatua hizo.

Bei ya mafuta ulimwenguni imeongezeka kwa viwango vya juu sana kwa sababu ya vita kati ya Russia na Ukraine, na kusababisha ongezeko la gharama ya maisha na usafiri kwa namna ambayo imeathiri sana nchi za Afrika magharibi kama Ghana.

Serikali ya Ghana inasumbuka pia kuongeza kodi ya mapato ya ndani wakati bunge limeshindwa tangu mwaka jana kupitisha mswada wa sheria wenye utata, wa kuongeza kodi ya asilimia 1.75 kwa lengo la kuongeza mapato ya serikali.

“Ni muhimu kusisitiza wazi kwamba, matatizo tunayokabiliana nayo nchini Ghana si ya Ghana pekee”, taarifa ya waziri wa fedha imesema.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa “Serikali katika nchi tajiri na nchi maskini zote zinashughulika na kuja na maagizo ya kufufua tena uchumi wao, baada ya athari mbaya za Covid 19 ambazo zilidumaza usambazaji wa bidhaa kote ulimwenguni, bila kusahau vita vinavyoendelea kati ya Russia na Ukraine.”

Hatua nyingine ni kupunguza kwa asilimia 50 ruzuku ya mafuta iliyokuwa inapewa wateule wa kisiasa na wakuu wa taasisi za serikali.

XS
SM
MD
LG