Serikali hiyo chini ya uongozi wa waziri mkuu mpya Gervais Ndirakobuca, ina mawaziri wapya watano, miongoni mwao ni waziri wa usalama na mambo ya ndani Martin Ninteretse na waziri wa fedha Audace Niyonzima ambaye amechukua nafasi ya waziri Domitien Ndihokubwayo, aliyehudumu kwenye uadhifa huo tangu mwaka wa 2016 chini ya utawala wa hayati rais Pierre Nkurunziza.
Baraza hilo jipya lina mawaziri 15, sawa na baraza la hapo awali, amri ya rais imeonyesha.
Jumatano, rais Ndayishimiye alimsimamisha kazi waziri mkuu Guillaume Bunyoni, bila pamoja na hivo kueleza sababu za kuchukua hatua hiyo.
Lakini wiki iliyopita, Ndayishimiye alisikika akionya kwamba “kuna watu ambao wanadai ni vigogo serikalini, wanaopanga njama ya kuniondoa madarakani,” alisema, akiwa katika mkoa wa kisiasa wa Gitega.
Ndayishimiye alichukua hatamu za uongozi mwezi Juni mwaka wa 2020, kumrithi mtangulizi wake Pierre Nkurunziza, baada ya uchaguzi wa kutatanisha ambao matokeo yake yalipingwa na chama kikuu cha upinzani cha National Congress for Liberty (CNL), kinachoongozwa na mbunge Agathon Rwasa.