Rais wa Algeria Abdelmadjid Tebboune amelazwa katika hospitali ya kijeshi kwa matibabu maalum, siku chache kabla ya kufanyika kura muhimu ya maoni kuhusu k marekebisho ya katiba, ambayo anataka yafanyike.
Taarifa kutoka ofisi ya rais haijaeleza wazi iwapo rais Abdelmadjid Tebboune ameambukizwa virusi vya Corona, lakini hali yake inaripotiwa kuwa imara na kwamba alikuwa anaendelea kufanya kazi.
Tebboune, mwenye umri wa miaka 75, alisema Jumamosi kwamba alikuwa amejiweka karantini baada ya maafisa wa ngazi ya juu walio karibu naye kuambukizwa virusi vya Corona.
“Nawaahidi ndugu na dada zangu kwamba afya yangu ni nzuri na kwamba naendelea kufanya kazi zangu kama kawaida,” alisema Tebboune.
Iwapo itathibitishwa kwamba anaugua corona, Tabboune ataingia katika kundi la viongozi duniani ambao wameugua virusi hivyo akiwemo rais wa Marekani Donald Trump, waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson na rais wa Brazil Jair Bolsonaro.
Tebboune amelazwa hospitalini wakati ambao ni muhimu sana kwake kuendelea na juhudi za kuleta mabadiliko nchini humo baada ya maandamano ya mwaka uliopita, yaliyouangusha utawala wa miaka 20 wa Abdelaziz Bouteflika.
Tebboune, ambaye alichaguliwa mwezi December mwaka uliopita, anataka nchi hiyo kuwa na katiba mpya, itakayoweka kikomo kwa muhula wa rais madarakani, na bunge pamoja na mahakama kuwa na mamlaka makubwa.
Kura ya maoni kuhusu Katiba hiyo inatarajiwa kufanyika Jumapili wiki hii.
Uchumi wa Algeria umeathirika sana kutokana na janga la virusi vya Corona.
Mapato kutoka kwenye mafuta na gesi yamepungua kwa kiasi kikubwa na hivyo kuathiri shughuli kadhaa za serikali.
Kufikia sasa, watu 55,000 wameambukizwa virusi vya Corona na 2,000 kufariki.
Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC