Rais wa Uganda Yoweri Museveni ametangaza kifo cha Spika wa Bunge la Uganda, Jacob Oulanyah Jumapili akieleza kuwa “Alikuwa kada mzuri nimechelewa kutoa taarifa ili Watoto wake wajulishwe kwanza”.
Sababu ya kifo cha Oulanyah haijaelezwa, lakini alikuwa nchini Marekani akipatiwa matibabu kwa zaidi ya mwezi mmoja.
Oulanyah alichukua kiti cha Spika wa Bunge la Uganda Mei mwaka 2021 na kabla ya hapo alikuwa Naibu Spika kuanzia 2011.
Hayati Oulanyah alionekana mara ya mwisho Bungeni Disemba 2021, alipoongoza vikao vichache ikiwemo kile kilichopitisha mswaada wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), kilichopitisha haki ya wanachama kuweza kuchukua mafao yao wanapofikia nusu ya kipindi kabla ya kustaafu.
Oulanyah alikwenda nje ya nchi kupatiwa matibabu hapo Februari 4, huku kukiwa na taarifa zinazodai kuwa ndege ya shirika la ndege la Uganda yenye usajili code 5X-NIL ilitumika kumsafirisha hadi Seattle, Washington nchini Marekani. Safari hiyo ilikadiriwa kugharimu dola za kimarekani 500,000 (Shs 1.7b).
Safari ya Spika kupelekwa kwa matibabu nchini Marekani iliwakasirisha raia wa Uganda wanaoishi Marekani wakipinga matumizi hayo kwa ajili ya safari hiyo.
Spika Oulanyah alizaliwa katika Wilaya ya Gulu, Machi 23, 1965 katika familia ya Nathan L'okori na Karen Atwon. Alisoma shule zifuatazo St. Joseph's College Layibi, Dr Obote College Boroboro, na Kololo Senior Secondary School kwa masomo ya O-Level na A-Level education.
Mwaka 1988, alijiunga na Chuo Kikuu cha Makerere, na kusomea fani ya uchumi wa kilimo. Alihitimu mwaka 1991. Baadae alijiunga na kitengo cha Sheria na kupata shahada ya Sheria mwaka 1994.