Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Juni 14, 2024 Local time: 18:24

Rais Mpya wa Somalia Atapigania Wananchi Wake Waingie Marekani


Rais wa Somalia, Mohamed Abdullahi Farmajo
Rais wa Somalia, Mohamed Abdullahi Farmajo

Rais mpya wa Somalia, Mohammed Abdullahi Farmajo amesema atafanya jitihada ili nchi yake iondolewe katika orodha ya nchi ambazo raia wake wanaweza kuzuiliwa kuingia Marekani.

Mohamed Abdullahi Mohamed maarufu kama “Farmajo” ameiambia VOA kuhusu mkakati wake katika mahojiano ya simu Alhamisi, siku moja baada ya ushindi uliokuwa haujategemewa katika uchaguzi wa rais uliofanyika Somalia.

“Ni sehemu ya jukumu langu kuzungumzia suala hili na uongozi wa Marekani. Nitampelekea ujumbe wetu rais wa Marekani na serikali yake kwamba watu wa Somalia ni wema, na wenye kufanya kazi kwa bidii,” amesema Farmajo.

“Wasomali wameendelea kukuza familia zao huko Marekani. Hivyo tutaona iwapo anaweza kubadilisha sera hiyo na kuiondoa Somalia kutoka kwenye orodha ya waliozuiliwa kuingia Marekani.”
Mustakbali wa amri ya kiutendaji “inayozuia wahamiaji” umeingia mashakani baada ya Mahakama ya Rufaa kukubaliana na maamuzi yaliyotolewa na mahakama ya chini ambayo ilizuia kutumika kwa amri hiyo.

Hapo awali amri hiyo ya Rais Donald Trump ilisitisha kwa muda programu ya kuwatafutia makazi wakimbizi na kuzuia wasafiri kutoka Somalia na nchi sita zenye waislamu wengi kuingia Marekani.

Rais Trump ameahidi kupitia ujumbe wa Twitter kupinga maamuzi hayo ya mahakama, akionyesha kuna uwezekano wa uongozi wake kupambana kisheria.

Farmajo ana uraia pacha wa Marekani na Somalia, ametumia sehemu kubwa ya ujana wake Marekani, wakati mwingi akiwa magharibi ya jiji la Buffalo.

Hilo halijawazuia wabunge wa Somalia kumchagua siku ya Jumatano badala ya kiongozi aliyekuwepo madarakani Hassan Sheikh Mohamud na wagombea wengine 20 na yeye kuwa rais wa tisa wa nchi hiyo.

Farmajo ameiambia VOA kipaumbele chake cha kwanza ni kumchagua waziri mkuu mpya ambaye atashughulikia masuala ya kiusalama na migogoro inayojitokeza ya kibinadamu.
“Kuna tatizo kubwa la ukame kila mahali Somalia ambalo litasababisha njaa,” amesema.

Tutaendelea kuomba kwa jumuiya za kimataifa ziendelee kutusaidia misaada ya dharura inayohitajika katika maeneo yaliyoathirika nchini Somalia, amesema rais.

Kufuatia misimu miwili ya ukosefu wa mvua za kutosha, nchi hiyo tayari inakabiliwa na ukame na Umoja wa Mataifa imeonya kuwa kuna uwezekano mkubwa ikatokea ile njaa ya mwaka 2011 iliyowauwa watu zaidi ya 250,000 .

Rais amesema kuwa anategemea kuwa waziri mkuu atachagua baraza lake la mawaziri katika siku 30, na wataelezea mipango kazi yao katika kipindi cha siku 100.
Lakini pia amekiri kwamba bado anajaribu kukabiliana na mazingiramapya katika nafasi yake ya uongozi.

XS
SM
MD
LG