Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Aprili 25, 2024 Local time: 03:26

Rais Kenyatta anatarajiwa kutia saini mswaada wa Marekebisho ya Vyama vya Siasa


Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta akizungumza kwa njia ya mtandao.
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta akizungumza kwa njia ya mtandao.

Rais Uhuru Kenyatta anatarajiwa wiki hii kutia saini muswaada wa Marekebisho ya Vyama vya Kisiasa kuwa sheria baada ya bunge la Seneti kuupitisha bila marekebisho kwa kura ya Maseneta 28 dhidi ya 3, Jumatano jioni katika kikao maalum cha bunge hilo.

Mswaada huo ulihitaji angalau maseneta 24 waliochaguliwa kupiga kura kuunga mkono ili upitishwe.

Hii ni licha ya juhudi za dhati za Maseneta wanaoegemea naibu rais William Ruto katika chama chake cha United Democratic Alliance (UDA) kupendekeza marekebisho 15 kwenye mswaada huo. Wakati wakijadili katika kikao hicho kilichodumu zaidi ya saa tano, wabunge hao wameutaja Mswaada huo kama chombo kilichoundwa kukidhi maslahi ya kisiasa ya ubinafsi, na kwamba pia unahitilafiana na majukumu ya tume ya uchaguzi, IEBC.

Mswaada huo unarasimisha uundaji wa miungano ya kisiasa nchini humo kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9 mwaka huu.

Wabunge wanaomuunga mkono rais Kenyatta na mwenzake katika maridhiano ya kisiasa Raila Odinga, wameonekana kuridhishwa na vipengele mbalimbali kama vile kipengele cha nane(b) kinachopendekeza vyama vya kisiasa kuwasilisha kwa msajili wa vyama mkataba wa muungano wa vyama vya kisiasa miezi minne kabla ya uchaguzi mkuu.

Iwapo rais Kenyatta atatia saini Mswaada huo na kuufanya kuwa sheria, vyama vya kisiasa vina hadi Aprili mwaka huu kuwasilisha hati za makubaliano ya mkataba muungano wa vyama vya kisiasa kwa msajili wa vyama vya siasa.

Kipengele cha 10 katika Muswaada huo kinapendekeza viongozi waliochaguliwa kuwa watiifu kwa itikadi na falsafa ya chama kilichowapeleka uongozini hadi wakati wanapokamilisha muhula wao au kujiuzulu kwa mujibu wa sheria ya vyama.

Kifungu cha 22 cha Mswaada huo vile vile kinampa mamlaka zaidi msajili wa vyama vya siasa nchini Kenya, ikiwa ni pamoja na kuthibitisha kwamba majina ya watu kwenye orodha ya vyama ni wanachama halisi wa chama fulani, mamlaka ya kusimamia uteuzi katika vyama vya kisiasa na kutoa orodha iliyoidhinishwa ya wanachama kushiriki katika mchakato huo.

Vifungu vingine vinahusu mtindo wa kuendesha kura za mchujo wa vyama, kama vile uteuzi wa moja kwa moja au njia nyingine zilizopo kwenye sheria.

Kupitishwa kwa Mswaada huo kunatajwa kuwa ushindi mkubwa na nguvu mpya kwa rais Kenyatta na Odinga, na utekelezaji wake sasa utatoa mwanga wa kubuniwa kwa muungano wa kisiasa chini ya Muungano wa Azimio la Umoja ambao unaongozwa na kinara wa ODM Raila Odinga na kuungwa mkono na rais Kenyatta.

"Ninapongeza kupitishwa kwa Mswaada huu kwa sababu unatoa mfumo wa kuanzisha miungano na kuifanya iwezekane kufanya kazi," ameeleza Seneta wa jimbo la Siaya, James Orengo ambaye pia ni Kiongozi wa Wachache bungeni humo.

Wabunge wanaoegemea upande wa William Ruto, ambao wamepinga vikali Mswaada huo, hata hivyo, wamepoteza kura ya kufanyia marekebisho vipengele vinavyohusu uundaji wa miungano ya kisiasa, muda wa kurasimisha miungano hiyo, kura za mchujo wa vyama, jukumu la msajili wa vyama vya kisiasa na vile vile mikakati ya kuhimiza nidhamu kwenye vyama hivyo.

“Tunaweka vizingiti vingi dhidi ya vyama vya siasa. Tutateseka na tutakumbuka haya baadaye,” amesema Kipchumba Murkomen, Seneta jimbo la Elgeyo Marakwet.

Spika wa bunge la Seneti Ken Lusaka atawasilisha Mswaada huo kwa Bunge la Kitaifa ambapo Spika Justin Muturi ataukabidhi kwa Rais Kenyatta ili audhinishe kuwa sheria, wiki chache tu baada ya bunge hilo kuupitisha katika kikao kilichogeuzwa kuwa uwanja wa masumbwi.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu wa Nairobi, Kennedy Wandera.

XS
SM
MD
LG