Rais wa China Hu Jintao amefanya mazungumzo na rais wa Sudan Omar- al Bashir baada ya kumpa makaribisho ya kirafiki nchini mwake.
Rais Bashir anakabiliwa na waranti ya kimataifa ya kukamatwa kwa tuhuma za uhalifu dhidi ya binadamu.
Katika hotuba ya ufunguzi katika ukumbi wa Great Hall of the People Jumatano , bwana Hu, alisema anatarajia ziara hiyo itaboresha uhusiano baina ya China na Sudan na kuongeza ushirikiano wa kibiashara katika nyanja mbalimbali.
Viongozi hao wawili baadaye waliungana na maafisa wengine kutia saini mikataba ya mkopo na ushirikiano wa kiuchumi .
China ni muuzaji mkubwa wa silaha nchini Sudan na mnunuzi mkubwa wa mafuta yake.
Wakati wa mkutano wao, marais hao wawili walitia saini makubaliano ya ushirikiano wa kiteknolojia pamoja na ujenzi wa daraja mashariki mwa Sudan.
Siku ya Jumanne kampuni ya kitaifa ya mafuta ya China ilitia saini makubaliano ya ushirikiano na Sudan, lakini hapakutolewa maelezo zaidi juu ya makubaliano hayo.