Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Machi 28, 2024 Local time: 14:56

Raila Odinga asema uchaguzi hautafanyika iwapo IEBC haitimizi matakwa yake


Mgombea wa urais nchini Kenya Raila Odinga akiwa na mgombea mwenza wake Martha Karua. May 16 2022. PICHA: AFP
Mgombea wa urais nchini Kenya Raila Odinga akiwa na mgombea mwenza wake Martha Karua. May 16 2022. PICHA: AFP

Mgombea wa urais nchini Kenya Raila Odinga, ametishia kutoshiriki uchaguzi mkuu wa mwezi ujao, endapo tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC haitatumia daftari la wapiga kura iliyoandikwa kwa karatasi na sio kutegemea orodha ya wapiga kura iliyotayarishwa kidigitali.

Odinga, ambaye katika uchaguzi uliopita 2017 alitaka upigaji kura kufanyika kwa njia ya digitali, amesema kwamba endapo IEBC haitatumia daftari la wapiga kura la karatasi, “uchaguzi hautafanyika.”

“Daftari la wapiga kura lazima litumike katika kila kituo cha kupigia kura. Hili halina mjadala na tumewaambia IEBC kwamba ni lazima tuwe na daftari la wapiga kura lililotayarishwa kwa karatasi, pamoja na majina hayo kupatikana kielektroniki ambapo wapiga kura watatambuliwa kwa alama za vidole au picha. La sivyo, hakuna uchaguzi,” amesema Odinga.

Kenya itaandaa uchaguzi mkuu mwezi ujao Agosti tarehe 9. Odinga, ambaye alitoa madai kama hayo katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2017, amedai kwamba kuna njama ya kutumia karatasi za kura ambazo tayari zimejazwa kwa faida ya mpinzani wake.

“Wamechagua vituo vya kupiga kura kama 10,000 ambavyo wataweza kuingiza hizo kura mia mbili mia mbili, ili ziingie pale ndipo wapate kura milioni mbili za ziada ya uongo.” Amedai Odinga ambaye anagombea urais kwa tiketi ya muungano wa vyama vingi, Azimio.

Odinga anaungwa mkono na rais wa sasa Uhuru Kenyatta na baraza lake la mawaziri

Odinga anaungwa mkono na serikali ya sasa ya rais anayeondoka Uhuru Kenyatta, ambaye alimshutumu katika uchaguzi uliopita kwa wizi wa kura, na kupelekea joto kubwa la kisiasa hadi walipokutana na kuingilia makubaliano ya kushirikiana kufanya kazi, maarufu nchini Kenya kama ‘handshake’.

Mpinzani mkuu wa Raila Odinga ni naibu rais William Ruto, ambaye amesema kwamba yupo tayari kwa uchaguzi na hana malalamiko yoyote na tume huru ya uchaguzi IEBC.

Ruto amesisitiza kwamba tume ya uchaguzi iruhusiwe ifanye kazi yake na mfumo wowote ule utakaotumika kufanikisha uchaguzi, uwe wa karatasi au elektroniki, hana shida nao.

“Hata washindani wangu wakimteua ndugu yao kuwa mwenyekiti wa tume ya uchaguzi IEBC, sina shida bora ateuliwe kulingana na sheria na uchaguzi uwe huru na wa haki” alisema Ruto katika kikao kati ya maafisa wa tume ya uchaguzi na wagombea wote wa urais.

Tume ya uchaguzi yajibu madai ya wizi wa kura

Mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC, amemjibu Raila Odinga, akisema kwamba tume hiyo haifanyi kazi kwa kuzingatia maslahi ya mtu binafsi na haiwezi kubadilisha sheria za uchaguzi ili kutosheleza mahitaji ya mtu mmoja.

“IEBC ni tume huru, hatupokei maagizo kutoka kwa mtu binafsi, mamlaka yoyote au taasisi yoyote. Kazi yetu inazingatia katiba na sheria za Kenya,” amesema mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati, akiongezea kwamba “unaweza kutofurahishwa na namna tunavyofanya kazi lakini iwapo tunafuata sheria katika kazi yetu, hatuwezi kuwa na wasiwasi. Tunafanya kazi yetu bila uoga wala upendeleo, na kwa kuzingatia sheria.”

Chebukati amesema kwamba kila kituo cha kupigia kura kitakuwa na daftari la mpiga kura, na idadi ya karatasi za kupigia kura zitakuwa sawa na idadi ya wapiga kura waliosajiliwa katika kila kituo.

Mkurugenzi wa IEBC Majan H. Marjan, amesema kwamba "Tume ya uchaguzi IEBC inafanya kazi yake kwa kuzingatia uamuzi wa mahakama ya juu kabisa wa mwaka 2017 kwamba daftari la wapiga kura ambalo linastahili kuzingatiwa kabisa ni la kidigitali na daftari la karatasi litumike tu iwapo kuna hitilafu katika mfumo wa digitali." ameongezea kwamba "daftari la karatasi linachapishwa kutoka kwa lile la digitali."

Madai ya uchapishaji wa karatasi za kupiga kura kuingiliwa na wapinzani wa Odinga

Raila Odinga vile vile amedai kwamba kampuni iliyopewa kandarasi ya kuchapisha karatasi za kupiga kura ina uhusiano na wapinzani wake.

Seneta wa Bungoma Moses Wetangula ametajwa aliwahi kukutana na baadhi ya watu wenye uhusiano na kampuni ya Ugiriki ya Lykos (Hellas) SA Holdings, ambayo ilishinda zabuni ya kiasi cha shilingi bilioni 3 ya kuchapisha karatasi za kupigia kura. Zabuni ilitolewa mwezi Oktoba mwaka 2021.

Ripoti ya gazeti la Daily Nation la Kenya, hata hivyo haiunganishi moja kwa moja, uhusiano kati ya watu ambao Wetangula alikutana nao, na kampuni hiyo. Hata hivyo, ripoti hiyo imezua mjadala mkubwa wa kisiasa nchini Kenya.

Wetangula, ambaye ni wakili, na alikuwa rafiki mkubwa wa kisiasa wa Raila Odinga hadi walipokosana miaka michache iliyopita, ni mmoja wa maafisa wakuu katika kampeni ya naibu rais William Ruto, na ambaye ni mshindani mkubwa wa Odinga.

Wetangula amemjibu Raila na chama chake kwamba “tunataka kuwaambia washindani wetu wanaoitwa Azimio kuacha kuonyesha wasiwasi kila mara na kila sehemu kwa sababu inaonekana kwamba Azimio wako katika hali ya kuchanganyikiwa pamoja na kuwa na misukosuko ndani ya chama chao na sasa wameanza kudai kwamba kuna njama za kuwaibia kura.”

Wetangula amedai kwamba Odinga ana tabia ya kulalamika katika kila uchaguzi, akiitaja miaka ya 1997, 2007, 2013 na 2017.

“Nimesoma vizuri na kwa makini habari zilizochapishwa. Sina msaidizi anayeitwa Joshua. Sina uhusiano na mtu yeyote anayefanya biashara ya uchapishaji. Watu ambao wanatajwa hata siwajui,” amesema Wetangula katika taarifa kwa vyombo vya habari.

Mwenyekiti wa IEBC atajwa katika madai hayo

Mwenyekiti ya tume ya uchaguzi Wafula Chebukati, vile vile ametajwa na wanasiasa kwamba alifanya mikutano na Wetangula na wanasiasa wengine wanaomuunga mkono William Ruto kabla ya zabuni ya kuchapisha karatasi za kupiga kura kutolewa.

“Inasikitisha sana kwamba kuna watu wanasema mambo kama hayo. Sijawahi kuketi chini na mtu yeyote kujadiliana maswala ya kutoa zabuni ya kuchapisha karatasi za kupiga kura.” Amesema Chebukati huku wanasiasa wanaomuunga mkono Raila Odinga wakitaka taasisi za serikali kufanya uchunguzi wa haraka.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG