Odinga aliyatangaza hayo alipowahutubia waandishi wa habari mjini Nairobi.
"Baada ya kutafakari msimamo wetu kuhusiana na uchaguzi ujao, tumeangalia maslahi ya watu kenya, eneo na dunia kwa ujumla, tunaamini kwamba itakuwa ni vizuri sana kama chama chetu kumuondoa mgombea wa urais katika uchaguzi wa October 26," Odinga aliuambia mkutano wa wana habari leo jumanne.
Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 72 alisema kuna kila dalili kuwa uchaguzi uliopangwa utakuwa mbaya zaiddi kuliko ule uliofanyika tarehe nane mwezi Agosti.
Na akizungumza muda mfupi baada ya Odinga kutangaza kujiondoa, rais Uhuru Kenyatta, ambaye ndiye mgombea wa chama cha Jubilee, alisema kwamba kampeni zake zitaendelea na wafuasi wake watashiriki katika uchaguzi wa tarehe 26.
Alionyesha kumshangaa Odinga kwa kusema: "Nasikia sasa umesema umejitoa. Baada ya kutupeleka na kutupeleka, ziadi ya shilingi bilioni 12 zimetumika tufanye uchaguzi..pesa ambayo tungetumia kujenga hospitali za wananchi...na sasa amesema hataki. Sisi twasema tuko tayari, awepo asiwe."
Kenyatta hata hivyo alisema ni haki yake ya kikatiba kujiondoa kwenye kinyang'anyiro hicho lakini akaongeza kuwa Wakenya wengine pia wana hakai ya kushiriki kwenye zoezi hilo.
Haya yamejiri wakati wabunge wa mrengo wa upinzani wakisusia vikao vya kamati ya bunge kuhusu azma ya ubadilishaji wa sheria ya uchaguzi.
Mahakama ya juu awali ilibatilisha matokeo ya upigaji kura wa agosti 8 - ambapo rais aliyekuwepo madarakani uhuru Kenyatta alitangazwa mshindi - kutokana na dosari zilizojidhihirisha kwa upande wa tume ya uchaguzi na mipaka.
Baada ya taarifa ya kujiondoa kwa Odinga, IEBC iliandika kwenye mtandao wake kwamba makamishna wake walikuwa wanakutana kutadhimini mwelekeo.