Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Februari 07, 2023 Local time: 22:15

Raia wa Rwanda wapatwa na wasiwasi nchini Uganda


Ramani ya Uganda na Rwanda

Mzozo kati ya Uganda na Rwanda unaendelea kushika kasi kutokana na kitendo cha baadhi ya Wanyarwanda kukamatwa Uganda na kurejeshwa Rwanda.

Mmoja wao aliyerejeshwa Rwanda amezituhumu ngazi za upelelezi za Uganda kuhusika kwenye kamata kamata hiyo.

Mwandishi wa idhaa ya Kiswahili VOA ameripoti kuwa Emmanuel Kemayire aiyekuwa akiendesha shughuli zake za biashara kwenye mji wa Mbarara magharibi mwa Uganda anasema alikamatwa tarehe Januari 4, 2018 na kufungwa vitambaa usoni na kusafirishwa usiku hadi mjini Kampala.

Walinikaba majira ya usiku na kunifunga kitambaa usoni ili nisijue chochote kinachoendelea na kunipeleleka, Kampala.

“Tulifika Kampala kama saa saba usiku,walinipeleka kwenye gereza la Mbuya na kunifunga pingu huku nikiwa nimening’inizwa miguu hewani. Hii imeniathiri kwa sababu mpaka sasa naumwa mgongo kutokana na kwamba siku hizo zote nilikuwa nikilala sakafuni. Hata macho hayaoni vema maana siku zote nilifungwa vitambaa usoni,” alisema.

Emanuel Kemayire ni raia wa saba wa Rwanda kukamatwa na kurejeshwa Rwanda baada ya kuwekwa kizuizini kwa kile wao wanachoeleza ni hatua za upelelezi za nchini Uganda.

Mwezi Disemba mwaka 2017 walirejeshwa nchini kwa nyakati tofauti raia sita wa Rwanda akiwemo mmoja aliyekamatwa wakati akimtembelea mtoto anayesoma chuo kikuu nchini Uganda.

Wakati huo watu hao walitaja kwamba walikamatwa na maafisa wa upelelezi wa Uganda ambao kama walivyodai raia hao wa Rwanda, ngazi hizo za upelelezi za Uganda zilishirikiana na kundi la wakereketwa wa kundi la RNC, linaloongozwa na Luteni Jenerali Kayumba aliyewahi kuwa mkuu wa jeshi la Rwanda kwa sasa akiwa ukimbizoni nchini Afrika Kusini.

Emmanuel Kemayire anaeleza: “Kwa muda huo wote nilikuwa nijitetea huku wakiendelea kunitesa na kuniuliza maswali mengi.Lakini niliendelea kuwaeleza kuwa mimi sikuwa na uhusiano wowote wa kisiasa, lakini hatimaye baada ya kuchunguza nyaraka zangu zote..simu za mkononi na ujumbe wake na mambo mengine walinieleza kuwa waliridhika na maelezo yangu kisha wakaniachia huru.”

Kemayire alitoa maelezo hayo makao makuu ya polisi mjini Kigali siku moja baada ya kurejeshwa kutoka Uganda. Hata hivyo msemaji wa jeshi la polisi la Rwanda amejizuia kutamka lolote juu ya mkasa huu.

Lakini hapo awali balozi wa Rwanda nchini Uganda Frank Mugambage alithibitisha kuwa ubalozi wa Rwanda ulikwisha iandikia barua serikali ya Uganda huku wakiomba maelezo ya visa vinavyowapata raia wa Rwanda walioko Uganda.

Wakati haya yanajiri Raia wa Rwanda wanaosafiri kwenda Uganda wameendelea kuwa na wasiwasi wa kile kitakachowapata iwapo nchi hizo mbili hazitafikia makabiliano ya wazi.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Sylvanus Karemera, Rwanda

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG