Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Februari 09, 2023 Local time: 05:02

Wachambuzi: Jeshi la Afrika mashariki haliwezi kuleta amani DRC


Kamanda wa kundi la waasi la M23 Generali Sultani Makenga, akiwa katika kikao na waandishi wa habari, Bunagana, Mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo. Sep 2013. PICHA: REUTERS

Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo imefunga kabisa shughuli za biashara kwenye mpaka wake na Uganda wa Bunagana. Hatua hiyo imechukuliwa saa chache baada ya viongozi wa DRC, Kenya, Rwanda, Uganda na Burundi kukutana Nairobi kuweka mikakati namna ya kupambana na makundi ya waasi mashariki mwa DRC.

Waasi wa M23 waliuteka mji wa Bunagana baada ya kuwashinda nguvu wanajeshi wa DRC, ambao walilazimika kukimbilia Uganda.

Gavana wa Kivu kaskazini Luteni Generali Ndima Kongba, ametangaza kwamba kivuko cha Bunagana kimefungwa kwa mda usiojulikana, na hakuna bidhaa kuingia au kutoka kupitia huko.

Taarifa ya Gavana Ndima imesema kwamba mtu yeyote atakayefanya biashara kwa njia haramu kupitia Bunagana, atakabliwa vikali kisheria.

Waasi wa M23 walitangaza kuufungua kivuko hicho cha mpakani siku ya jumatatu na serikali ya Kinshasa ilitangaza Jumanne kukifunga tena leo, kivuko hicho.

Makubaliano ya marais wa Afrika mashariki

Marais wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Uhuru Kenyatta wa Kenya, Yoweri Museveni wa Uganda, Salva kiir wa Sudan kusini, Felix Tshisekedi wa DRC, Everiste Ndayishimiye wa Burundi na Paul Kagame wa Rwanda, walikubaliana katika kikao cha Jumatatu wiki hii, kuharakisha kuundwa kwa jeshi la pamoja kupambana na waasi DRC. Lakini aliyekuwa mkuu wa idhara ya ujasusi kwa ajili ya usalama wa Uganda (ISO) Charles Rwomushana, anasema kwamba makubaliano hayo hayawezi kusuluhisha matatizo ya usalama ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.

“Watu waliohudhuria kikao cha Nairobi ndio wahusika wa vita katika jamhuri ya kidemokrasia ya Congo. Wanahusika na vita vya kutumia watu wengine nchini Congo. Katika taarifa yao baada ya kikao, hawajazungumzia hatua watakazochukua kutatua mgogoro kati ya rais wa Rwanda Paul Kagame na kiongozi wa kundi la waasi la FDLR Kayumba Nyamwasa, na Museveni pamoja na waasi wanaompinga wanaojificha DRC. Kama mambo hayo hayapati suluhu, Kagame anaamini kwamba Museveni anamunga mkono Nyamwasa, na uwanja wa fujo sasa ni Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.” amesema Rwomushana.

DRC imeendelea kudai kwamba Rwanda inaunga mkono waasi wa M23

Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo imeshutumu Rwanda kwa kuunga mkono waasi wa M23 wanaopigana na wanajeshi wa DRC na ambao sasa wamedhibithi Bunagana, mji muhimu sana kwa shughuli za kibiashara. Mpaka wa Bunagana unatumika na Kenya, Tanzania na Uganda kwa usafirishaji wa bidhaa kuingia DRC.

Balozi wa DRC nchini Uganda Jeane Pierre Masala aliambia vyombo vya habari vya Uganda kwamba Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo ilipata kiasi cha dola milioni 71 kutokana na biashara kupitia mpaka wa Bunagana, kufikia mwezi Januari mwaka huu 2022. Hii ina maana kwamba biashara ya Uganda pekee kuelekea DRC kupitia mpaka huo inaweza kufikia kiasi cha dola bilioni 1 katika kipindi cha mwaka mmoja. Uganda inauza DRC saruji, mafuta ya kupika, vifaa vya ujenzi, vinywaji ikiwemo pombe, na hivyo mpaka huo ni muhimu sana kwa Uganda.

Rwanda, imeshutumu DRC kwa kuunga mkono waasi wa FDLR wanaotuhumiwa kwa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994. Rwomushana anasema tatizo ni kubwa kulikoa tuhuma zinazotolewa na kila upande na kwamba yoye yanahusu kundi la FDLR na kamanda wake, Kayumba Nyamwasa.

“Kuwepo kwa kundi la Nyamwasa kunasababisha hali ngumu kwa sababu Nyamwasa alikuwa kamanda wa jeshi la Rwanda wakati Kagame na Museveni waliunda jeshi la pamoja ambapo lilijukilana kama Banyamulenge Force na ambalo lilimuondoa madarakati Mobutu na iwapo Nyamwasa alikuwa afanikiwe na juhudi zake ambazo ziliungwa mkono na Uganda, katika sehemu za Uvira, basi itakuwa shida kubwa kwa kagame kwa sababu mashariki mwa Congo ni muhimu sana kwa uchumi wa Rwanda na ndio wasiwasi mkubwa ya Kagame.” Ameeleza Rwomushana, aliyekuwa mkuu wa idhara ya usalama wa ndani ya Uganda (ISO).

M23 waliwahi kukimbilia Uganda na kupewa hifadhi katika kambi ya kijeshi

Kundi la M23 liliwahi kukimbia mapigano ya wanajeshi wa Monusco, Novemba 2013 baada ya kupigana kwa karibu miezi 19. Hatua hiyo ilitoa matumaini kwamba huenda waasi hao wangefikia makubaliano na serikali ya Congo, huku maelefu ya raia wa Congo wakiishi katika kambi za wakimbizi.

M23 na kamanda wao Sultan Makenga, walizuiliwa katika kambi ya kijeshi ya Mgahinga nchini Uganda, karibu na mpaka wa DRC.

Rwomushana anasema kwamba mapigano mashariki mwa DRC, yalitarajiwa.

“Siwezi kushangazwa na ripoti kwamba kuna kundi la waasi Bunagana linalohusishwa na Rwanda. Sio lazima liwe M23 kwa sababu kundi la M23 lipo kwa sababu lilinusurika mashambulizi ya Umoja wa Mataifa wakiwemo wanajeshi wa Tanzania. Kundi hilo lilikuwa chini ya kamanda Brigedia Makenga ambaye alikuwa mwanafunzi aliyeokolewa na Museveni. Kwa hivyo halitakuwa kundi la M23 ambalo linapinga malengo ya Museveni. Waasi ambao wamedhibithi Bunagana walipewa hifadhi na Museveni, japo hatujui kama linamuunga mkono Museveni au la. Kwa hivyo, hawa marais wamekuwa wakijenga makundi ya wapiganaji na waasi katika eneo la Kivu na makundi haya yanahama kutoka sehemu moja hadi nyingine.”

Wakaazi mashariki mwa DRC hawataki jeshi la Jumuiya ya Afrika Mashariki

Kulingana na shirika la habari la AFP, watu wengi mashariki mwa DRC hawataki Jumuiya ya Afrika Mashariki kutuma jeshi la pamoja kupambana na makundi ya waasi.

Hawana Imani na jeshi hilo ambalo viongozi wanapanga kuunda. Baadhi ya wakaazi hao wanasema kwamba baadhi ya majirani wa DRC wanajihusisha moja kwa moja na mapigano yanayoendelea DRC.

Kundi la wanaharakati wa haki za kiraia mjini Goma, LUCHA, limeandikia rais wa DRC Felix Tshisekedi barua kupinga hatua hiyo. Katika barua kwa Tshisekedi, kundi la Lucha limedai kwamba Uganda, Rwanda na Burundi, wanahusika katika vita vya DRC na ni makosa kudhani kwamba wanaweza kusaidia DRC. Romushana, anaunga mkono na msimamo wa kundi la Lucha na wakaazi wengine wa mashariki mwa Congo.

“Huwezi kusuluhisha mgogoro wa Congo kwa kutumia jeshi la pamoja kama la jumuiya ya Afrika mashariki, SADEC, au jeshi la umoja wa mataifa kwa sababu ukitumia nguvu za kijeshi, unaendelea tu kuongeza vita na kupelekea watu kukoseshwa makao. Hata hizi nchi zikiungana kijeshi au kila nchi iingie DRC kivyake kupambana kijeshi, hawawezi kufanikiwa kutokana na milima ya DRC na mgogoro wa kisiasa sehemu hiyo. Njia bora ni kufanya mazungumzo. Lakini huwezi kufanya mazungumzo iwapo hautahusisha waasi wa Nyamwasa kutoka Rwanda, na waasi wanaompinga rais Museveni wakiwemo waasi wa Allied democratic forces, ADF.”

Mapigano kati ya Rwanda na Uganda ndani ya DRC

Wanajeshi wa Uganda na Rwanda wamewahi kupigana kwenye ardhi ya Congo na kila nchi kupata hasara kubwa.

DRC imesema haitaki Rwanda kuwa sehemu ya jeshi la pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki ikidai kwamba Rwanda inaunga mkono waasi wa M23, madai ambayo Rwanda imekanusha mara kadhaa.

Jeshi hilo litashika doria sehemu za Kivu kaskazini, Kivu kusini, Ituri hadi sehemu za kaskazini.

Uganda tayari ina jeshi lake sehemu hiyo, linalopigana vita na kundi la waasi la Allied democratic forces ADF. Uganda pia inajenga barabara ndani ya DRC.

“Museveni anajenga barabara nchini Congo kwa ajili ya usalama, na wala sio kwa sababu ya biashara na uchumi. Barabara na mawasiliano yakiwa mabaya nchini Congo, ndivyo raia wa Congo watafanya biashara na Uganda. Wakipata barabara nzuri na viwanja vya ndege, watafanya biashara nchini mwao na kimataifa. Lengo hapa ni kuwalenga waasi. Swala kuu hapa ni kwamba tofauti kati ya Museveni na Kagame hazijawahi kusuluhishwa. Swala la Nyamwasa halijawahi kusuluhishwa.”

Waasi waamrishwa kuwacha vita

Mrais wa jumuiya ya Afrika mashariki waliwaamuru waasi walio mashariki mwa DRC kuweka chini silaha. Raia wa DRC wanasema kwamba jeshi la umoja wa mataifa MONUSCO, limeshindwa kuleta amani nchini humo.

Kama ilivyo na raia wengi wa DRC waliohojiwa, mshindi wa tuzo ya Nobel Denis Mukwenge, hana imani na jeshi hilo la Afrika Mashariki lililo na wanajeshi kutoka nchi ambazo zimeshutumiwa kwa kutatiza usalama wa DRC pamoja na wizi wa raslimali zake.

Rwomushana anasema kwamba ni vigumu kuwapokonya silaha waasi wa DRC.

“Huwezi kuzungumzia kuwapokonywa waasi silaha nchini Congo bila kuzungumzia kumaliza nguvu za Nyamwasa. Je, utapokonya Nyamwasa silaha na kumwezesha kuishi maisha ya kawaida nchini Rwanda? Hilo linawezekana? Unaweza kufanya hivyo bila kumhusisha Nyamwasa katika mazungumzo? Je, utawapokonya silaha waasi wanaompiga vita Museveni walio ndani ya nchi na nchini Congo? Na je, unaweza kufanya hivyo bila kuwahusisha katika mazungumzo ya moja kwa moja na Museveni? Kama huwezi kufanya hivyo kwa njia ya uwazi, basi huwezi kusuluhisha tatizo hilo. Kwa sasa, wanamaliza tu mda.”

Chuki za kikabila zimeongezeka DRC

Ujumbe wa chuki za kikabila umeenea mashariki mwa DRC.

Maafisa wa serikali ya DRC wamemshutumu mtoto wa rais Yoweri Museveni, ambaye ni kamanda wa majeshi ya nchi kavu wa Uganda Luteni Generali Muhoozi Kainerugaba, kwa kuchochea chuki za kikabila kwa kutumia ujumbe wa twiter, akiwapendelea watu wa kabila la Watutsi, Heema na Banyamulenge, ambao wengi wao wamo katika kundi la wapiganaji la M23.

Ujumbe wa Muhoozi ulipelekea baadhi ya wabunge wa DRC kutaka jeshi la Uganda, linalopigana na waasi wa ADF, kuondoka nchini humo.

Shutuma hizo zimepelekea Muhoozi kukoma kuandika ujumbe kama huo wa chuki za kikabila.

Muhoozi aliahidi kukabiliana na kundi la FDLR. Wachambuzi walitafsiri ujumbe wake kama wa kuunga mkono kundi la M23 na kupanga kushambulia kundi la FDLR.

“Linaloendelea ni vita kati ya Rwanda na Uganda kwa kutumia makundi ya waasi. Na wawili hao wanastahili kuwa wakweli na kusuluhisha tofauti kati yao na kuzungumza na makundi ya waasi yanayowapinga. Haya hayawezi kufanyika katika kikao cha marais wa jumuiya. Sioni namna Rwanda inaweza kusaini makubaliano ya mkutano ambao Rwanda inaambiwa ifanye mazungumzo na Nyamwasa na Museveni hawezi kusaini akiwambiwa afanye mazungumzo na waasi wanaompinga na wanaojificha Congo.” Amesema Charles Rwomushana.

Mikakati ya marais wa jumuiya ya Afrika mashariki itafaulu?

Marais wa jumuiya wameamuru waasi wa M23 kuondoka Bunagana haraka iwezekanavyo.

“Maamuzi ya marais yaliyofanyika Nairobi hayana maana yoyote kwa sababu yanazungumzia tu mapigano kati ya serikali ya Congo na waasi. Kumbuka kwamba uchaguzi haukufanyika katika maeneo ya Kivu katika uchaguzi uliopita nchini Congo kwa hivyo hakuna vile utawaambia watu wa huko kwamba wanastahili kuheshimu katiba ambayo haiwahusu kwa sababu hata haikuwapa haki ya kupiga kura.” Ameendelea kusema Rwomushana.

Nini Kifanyike DRC?

Wachambuzi wa maswala ya kidiplomasia wanataka Uganda kufanya mazungumzo na makundi ya waasi yanayoiandama serikali ya Museveni, huku Rwanda ikifanya hivyo na kundi la FDLR, iwapo wanataka mgogoro wa DRC kupata suluhu la kudumu.

“Tatizo la DRC ni Nywamwasa. Na Nyamwasa, kulingana na Rwanda, anaungwa mkono na Museveni. Kwa hivyo huwezi kutuma jeshi nchini Congo labda kama unasema kwamba jeshi hilo linakwenda kumsaka Nyamwasa. Hakauna vile utapata amani DRC bila kuangazia Nyamwasa katika mazungumzo. Kwa hivyo, ni lazima Rwanda ifanye mazungumzo na Nyamwasa, na Museveni afanye mazungumzo na makundi ya waasi yanayompinga yaliyo nchini Congo. Shida iliyo nchini Congo inashinda Congo na watu wa Congo. Inahusu majirani wa Congo. Ambao ni Uganda, Rwanda na Burundi na makundi yao ya waasi.”

Makundi ya waasi kutoka Rwanda, Uganda na Burundi yaliyo DRC

Zaidi ya makundi ya waasi 100 yanapatikana mashariki mwa DRC. Miongoni mwao ni kundi la waasi wa Red Tabara na National forces of Liberation wanaotoka Burundi, Democratic Forces of Liberation of Rwanda FDLR, kutoka Rwanda na Allied democratic forces ADF kutoka Uganda. Mapigano ya sasa yanaendeshwa na kundi la M23 linalodai ni raia wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.

“Je DRC imemfukuza Nyamwasa? Kama unampa makao Nyamwasa, mbona unadhani kwamba Rwanda haitachukua hatua dhidi yako?” ameuliza aliyekuwa mkuu idhara ya usalama ya Uganda Charles Rwomushana.

Kagame akasirishwa na ushauri wa mazungumzo na FDLR

Pendekezo la aliyekuwa rais wa Tanzania Jakaya kikwete kutaka serikali ya Rwanda kufanya mazungumzo na kundi la waasi la FDLR, nusra lisababishe mgogoro mkubwa wa kidiplomasia kati ya Rwanda na Tanzania katikati ya mwaka 2013.

Kagame alimjibu Kikwete hadharani, akisema "kuna watu wamekuwa na mambo ya kusema, wakitaka sisi tufanye mazungumzo na watu walioua watu wetu. watu wanazungumzia FDLR kwa mzaha tu. Na wanajua wanazungumzia haya makaburi ya watu wetu na kwamba waliowaua, tuna deni nao. Kwanza, nilinyamaza kwa sababu ya madharau niliyoyaona. sababu ya pili, niliona ni kama upuuzi kabisa na la tatu, niliona ni ujinga mtupu, la nne, kama ni tatizo la fikra ambalo nadhani ndio sababu kubwa kwa mtu yeyote kufikiria kuhusu hilo, basi ni heri libaki na wale walilo nalo."

Kikwete alijibu kupitia hotuba kwa Tanzania akisema "uhusiano unelekea kupata mtikisiko baada ya mimi kutoa ushauri kwa serikali ya Rwanda kuzungumza na mahasimu wao. Ushauri wangu niliutoa kwa nia njema kabisa kwani bado naamini kwamba kama jambo linaweza kumalizwa kwa njia ya mazungumzo, njia hiyo ni bora zaidi kutumika kuliko vita. Isitoshe ushauri ule nilioutoa pia niliutoa kwa serikali ya Congo, na niliutoa kwa serikali ya Uganda pale pale kwenye kikao kile. Pale pale rais Yoweri Museveni aliunga mkono kauli yangu. Rais wa Rwanda hakusema chochote pale mkutanoni baada ya kurudi nyumbani ndipo tukaanza kusikia maneno tuliyoyasikia."

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG