Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Februari 07, 2023 Local time: 11:02

Qatar yaaga mapema michuano ya Kombe la Dunia


Timu ya taifa ya Qatar ilipopambana na Ecuador katika mechi ya kundi A na kushindwa 2-0.

Timu ya taifa ya Qatar imekuwa ya kwanza kuaga mashindano ya kombe la dunia baada ya kufungwa na Senegal bao 3-1 siku ya Ijumaa katika uwanja wa  Al Thumama Doha Qatar.

Timu hiyo imeaga mapema kuliko ilivyotarajiwa na uweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza kutolewa kwenye michuano hiyo huku wakiwa bado na mchezo mmoja mkononi.Mabao ya Senegal-Simba wa Teranga yalifungwa na Boulaye Dia, Famara Diedhiou na Bamba Dieng.

Senegal wanahitaji hata hivyo kushinda mechi yao ya mwisho na Ecuador ili kujihakikishia nafasi ya kusonga mbele katika raundi ya 16 ya michuano hii.

Senegal imekuwa timu ya kwanza kutoka Afrika kupata ushindi katika michuano hii.

Kwa upande wake Uholanzi na Ecuador wapo katika nafasi nzuri ya kuweza kusonga mbele kwa kuwa kila mmoja wao wana pointi 4.

Nao Vijana wa Marekani walikutana na mahasimu wao Uingereza katika mchezo uliokuwa ukisubiriwa kwa hamu nchini Marekani na Uingereza ambapo wamarekani wakiwa katika sikukuu ya Thanksgiving walijazana kwenye baa mbali mbali kuangalia mchezo huo.

Timu ya Marekani ambayo ina vijana wengi wenye umri mdogo ikiongozwa na kapteni mwenye umri wa miaka 23 tu Tyler Adams ilipambana vikali na Uingereza timu ambayo imesheheni majina mengi makubwa katika kombe la dunia na kutoka nayo sare ya 0-0.

Marekani walifanya vyema dhidi ya timu nambari 5 duniani Uingereza, lakini hakuna timu iliyoweza kupata bao wakati timu hizo mbili zilipotoka sare ya 0-0 katika mchezo wa Kundi B wa Kombe la Dunia.

Nahodha wa kikosi cha Uingereza Harry Kane amesema amesikitika hawakufanya vizuri dhidi ya Marekani.

Marekani anahitaji ushindi kusonga mbele wakati Uingereza inahitaji droo.

Mechi za Jumamosi

Siku ya Jumamosi wawakilishi wengine wa Afrika timu ya taifa ya Tunisia itapambana na Australia, huku Tunisia ikipewa nafasi ya kushinda na wachambuzi wa soka kutokana na kiwango ilichokionyesha katika mechi yao ya kwanza na timu ya taifa ya Denmark ambapo walitoka sare tasa isiyo na magoli.

Na katika mechi nyingine ya kundi C siku ya Jumamosi Saudia Arabia ambayo ilifanya maajabu katika mchezo wa ufunguzi dhidi ya Argentina itakwaana na Poland inayoongozwa na mchezaji mkongwe Robert Lewandowski ambaye katika mchezo wao wa kwanza dhidi ya Mexico alikosa penati.

Katika mchuano huo wachambuzi wanaipa nafasi Poland kutokana na uzoefu mkubwa wa wachezaji wake lakini pia kikosi cha Saudi Arabia tayari kimefanya maajabu kwa hiyo ni nafasi yao ya kuendelea kuonyesha ubora wao dhidi ya Poland na Robert Lewandowski.

Katika mchezo mwingine Jumamosi mabingwa watetezi Ufaransa wanakwaana na timu ya Denmark mchezo huu unatarajiwa kuwa mkali na wa kusisimua hasa kwa sababu unazikutanisha timu mbili zenye uwezo mkubwa barani Ulaya ambapo Ufaransa ni mabingwa watetezi wa kombe la dunia na wakati huo huo Dernmark iliweka rekodi ya kufika robo fainali kombe la Ulaya 2004 na kufika robo fainali kombe la dunia 1998.

Na katika mchezo mwingine siku ya Jumamosi ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa ni kati ya Argentina na Mexico timu hizi mbili za Amerika kusini zina uhasama mkubwa.

Argentina imeishinda Mexico mara 16 na kutoka sare mara 14 na washabiki pia wan chi hizo wana upinzani mkali ambao utashuhudiwa katika mechi hii inayotarajiwa kuwa ya kuvutia siku ya Jumamosi.

Siku ya Jumapili timu ya taifa ya Japan Blue Samurai watapambana na Costa Rica waliojeruhiwa vibaya na Uhispania kwa goli 7-0 kwa hiyo wanahitaji kujikomboa.

Nao vijana wa Ubelgiji ambao walishinda mchezo wao wa kwanza wanapamabna na wawakilishi wengie wa Afrika Morocco. Vijana wa Croatia watakumbana na Canada ambao wanahitaji ushindi baada ya kupoteza mchezo wao wa kwanza wakati Uhispania watapambana na Ujerumani.

Mechi ya Uhispania na Ujerumani pia inasubiriwa kwa hamu ili kuona ni kitu gani Ujerumani watafanya baada ya kujeruhiwa na Japan katika mchezo wao wa kwanza bila kutarajiwa na wengi katika michuano ya mwaka huu ya kombe la dunia.

Imetayarishwa na Sunday Shomari Doha Qatar.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG