Ripoti ya kurasa 75 ya kundi la kutetea haki za binadamu, lenye makao yake mjini London, imetolewa wiki mbili kabla ya kuanza kwa mashindano ya kombe la dunia.
Wapenzi wa kandanda zaidi ya milioni 1.2 wanatarajiwa kuhudhuria mashindano hayo nchini Qatar.
Namrata Raju, mkurugenzi wa shirika la India la Equidem amesema kwamba wafuasi wa kandanda wanastahili kujua kuhusu matayarisho ya mashindano hayo.
"Mara nyingi, waajiri huwa wanachukua pasipoti za wafanyakazi kinyume cha sheria na sio tu nchini Qatar lakini katika nchi nyingi hatua ambayo kulingana na mfumo wa ufadhili wameanza kuleta mabadiliko. Lakini bado kuna pengo kubwa kwa kuzingatia yale wanayosema yamefanya kama mabadiliko katika sheria na yale wanayofanya."
Maafisa wa Qatar, wameshutumu wakosoaji kwamba wamekosa kutilia maanani mabadiliko yaliyofanywa na kwamba wana misimamo tofauti kuhusu taifa hilo la kwanza la kiarabu na la kiislamu kuandaa mashindano ya kandanda ya kombe la dunia.
Asilimia 95 ya wafanyakazi nchini Qatar ni raia kutoka nchi za nje.
Wamejenga viwanja na miundo msingi kwa kasi isiyo ya kawaida, baada ya Qatar kupata haki ya kuandaa mashindano hayo, mnamo mwaka 2010.
Miongoni mwa ujenzi huo ni viwanja vya michezo, mfumo wa reli ya mwendo wa kasi, barabara na hoteli.