Rais wa Russia Vladimir Putin amefanya mazungumzo ya simu na kiongozi wa muda wa Mali Assimi Goita, yaliyoangazia usafirishaji wa chakula, mbolea na mafuta kuelekea Mali.
Goita ameandika ujumbe wa Twiter akisema kwamba wamezungumzia namna Russia inavyoweza kuisaidia Mali kisiasa.
Goita aliingia madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi miaka miwili iliyopita na amekosolewa na mataifa Jirani Pamoja na nchi za magharibi kwa kuchelewa kuandaa uchaguzi mkuu.
Utawala wa Goita vile vile umeshutumiwa kwa ukandamizaji wa haki za kibinadamu na kushirikiana na mamluki wa Russia kupambana na makundi ya wapiganaji wa kiisalamu.
Wakati huo huo, Mali imesema kwamba wanajeshi wake 42 waliuawa katika shambulizi la wapiganaji wa kiislamu lililotokea Jumapili.
Maafisa wamesema kwamba wanajeshi 22 zaidi walijeruhiwa huku wapiganaji 37 wenye uhusiano na kundi la Islamic state waliuawa.
Shambulizi lilitokea katika mji wa Tessit, ulio katika eneo ambalo limekumbwa na mashambulizi ya mara kwa mara, karibu na mpaka wa Mali, Burkina Faso na Niger.
Maafisa wamesema kwamba shambulizi hilo ndilo baya zaidi kuwahi kutokea nchini Mali katika muda wa miaka 10.
Maelfu ya watu wametoroka sehemu hiyo. Watu milioni mbili wametoroka eneo la Sahel kutokana na ukosefu wa usalama.