Program ya kugundua uvamizi wa viwavi jeshi kabla ya wadudu hao kushambulia mimea, inaweza kuwasaidia wakulima kukabiliana na mdudu huyo kulingana na taarifa ya mwandishi wetu wa Kampala Halima Athumani, inayosomwa na Kennes Bwire.
Tayari Viwavi jeshi wamesababisha hasara ya mabilioni ya pesa kutokana na uharibifu wa mimea barani Afrika na wanatishia kusababisha hasara zaidi iwapo hawatadhibitiwa.
Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa FAO, kwa ushirikiano na Wizara ya Kilimo ya Uganda, linasema kwamba programu mpya ya kidijitali, kwa ajili ya kukabiliana na wadudu hao, itasaidia kukomesha uharibifu utokanao na viwavi jeshi.
“Lazima tusisitize kwamba programu hii ni ya kuisaidia jamii kugundua uvamizi wa wadudu aina ya viwavi jeshi kwa mapema. Mkulima mwenyewe lazima awe na uwezo wa kugundua iwapo wadudu hao wamevamia mimea yake pamoja na kufanya maamuzi kulingana na taarifa alizo nazo," anasema mshauri wa Mimea na Wadudu, Bahana John.
Wakulima wanaingiza taarifa walizo nazo kwenye program halafu wanaitumia kufanya hesabu itakayowawezesha kujua kiwango cha uharibifu ili kuchua hatua madhubuti.
Program hii ambayo ilizinduliwa mara ya kwanza nchini Madagascar na baadaye nchini Zambia, inatarajiwa kutumika katika nchi zilizo katika jangwa la sahara ambapo viwavi jeshi wameripotiwa.