Uingereza imekumbwa na wimbi la ghasia ambalo lilizuka mapema wiki iliyopita, baada ya wasichana watatu vijana kuuwawa kwa shambulizi la kisu kaskazini magharibi mwa nchi, na kupelekea taarifa zisizo sahihi kwenye mitandao ya kijamii, zikidai kuwa aliyetekeleza mauaji hayo ni mhamiaji wa kiislamu.
Waziri Mkuu Kier Starmer, mwendesha mashitaka wa zamani, anakabiliwa na mzozo wa kwanza tangu kushinda uchaguzi wa Julai 4, na amewaonya waandamanaji kuwa huenda wakakabiliwa na vifungo vya muda mrefu jela, wakati akijaribu kuondoa ghasia mbaya zaidi kuwahi kutokea Uingereza ndani ya miaka 13.
“Jukumu letu kuu ni kuhakikisha jamii zetu ziko salama,” amewaambia wanahabari. Mamia ya waandamanaji kwenye miji kadhaa nchini humo wamepambana na polisi, huku wakivunja madirisha ya hoteli ambazo zimewapatia makazi waomba hifadhi kutoka Afrika na Mashariki ya Kati, huku wakipiga kelele “waondoeni” na simamisheni boti,” wakiwa na maana ya kuzuia boti za wahamiaji zinazowasili nchini humo.
Forum