Polisi nchini Uganda wamewafyatulia gesi ya machozi mamia ya wanafunzi waliokuwa wakiandamana mjini Kampala kupinga pendekezo la kupandishwa kwa gharama za masomo.
Mkuu wa Polisi nchini humo, Kale Kaihura ameiambia Sauti ya Amerika kuwa polisi iliwalazimu kuutawanya umati kwasababu waandamanaji walikuwa hawajaijulisha mamlaka kuhusu mipango yao ya kuandamana.
Maandamano yalifanyika kwenye chuo kikuu cha Makerere na pia kuwajumuisha wafuasi wa upinzani ambao walimtaka Rais Yoweri Museve kuachia madaraka.
Kuna ripoti kwamba baadhi ya watu walijeruhiwa katika mapambano hayo, lakini idadi yao haijapatikana.
Jana Alhamisi, polisi walifyatua gesi ya machozi na risasi za mpira wakati wa maandamano ya upinzani mjini Kampala kupinga ongezeko la bei chakula na mafuta.
Dazeni ya watu walijeruhiwa wakati wa mapambano hayo, ikiwa ni pamojana kiongozi wa upinzani, Kizza Besigye ambaye alipigwa risasi ya mpira mkononi. Maandamano mengine yalifanyika katika mji wa Mashariki wa Jinja na mji wa Masaka kusinimagharibi mwa nchi. Huko polisi pia walitumia gesi ya machozi kuvunja maandamano hayo.
Wanafunzi wa chuo kikuu cha Makerere waandamana kupinga ongezeko la gharama za masomo.