Kikosi cha usalama barabarani nchini Tanzania kimethibitisha kwamba jumla ya watu 103 walifariki dunia kutokana na ajali kubwa nane za barabarani zilizotokea katika kipindi cha mwezi mmoja kati ya Machi 13 hadi April 12 mwaka 2015.
Takwimu hizo zilitolewa mbele ya waandishi wa habari jijini Dar Es Salaam siku ya Jumanne na mkuu wa kikosi cha usalama barabarani DCP Mohamed Mpinga wakati alipozungumzia ajali hizo za barabarani ambazo kwa kiasi kikubwa zimezusha mshtuko miongoni mwa watanzania.
Hata hivyo licha ya kuzungumzia hatua mbalimbali za kudhibiti ajali ikiwemo marekebisho ya mapungufu ya sheria ya makosa ya usalama barabarani, kamanda Mpinga alisema kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa na jeshi la polisi nchini humo pamoja na maoni ya wananchi juu ya ajali hizo ilibainika kuwa yapo mambo kadhaa yanayochangia kutokea kwa ajali za mara kwa mara ikiwemo wadau wa usalama barabarani kutowajibika ipasavyo katika maeneo yao ya kazi huku akitolea mfano abiria kutomripoti dereva anapokiuka kanuni za usalama barabarani, wamiliki kutowadhibiti madereva waliowaajiri pamoja na wakala wa barabara Tanroads kutoweka miundombinu bora ikiwemo kurekebisha maeneo yaliyoharibika kutokana na sababu mbalimbali.
Kamanda Mpinga alikiri kuwepo kwa mapungufu katika sheria za usalama barabarani ambazo wakati mwingine zimekuwa zikichangia kuwafanya madereva wasiwe na khofu pindi wanaposababisha ajali akitoa mfano kwamba faini wanazotozwa pamoja na adhabu wanazopewa.
Wakati huo huo Waziri wa mambo ya ndani nchini Tamzania Mathias Chikawe alitoa tahadhari kwa watanzania na kuwataka kutafakari kwa makini na kuepuka matukio yeyote yatakayovuruga amani wakati huu nchi ikielekea kwenye upigaji kura ya maoni na uchaguzi mkuu baadae mwaka huu huku akiwataka viongozi wa dini kuepuka kujiingiza kwenye masuala ya siasa.
Waziri Chikawe katika mkutano wake na waandishi wa habari huko Dar Es Salaam aliwatoa khofu wa-Tanzania juu ya hali ya usalama wa nchi wakati huu wa vitisho mbalimbali ya kiusalama katika nchi jirani huku akisema wanadhibiti ipasavyo uingiaji wa raia mbalimbali kutoka nje ya nchi.
Kumekuwepo na taarifa mbalimbali za vitisho vya kigaidi katika ukanda wa Afrika mashariki ambavyo vimezusha taharuki kubwa miongoni mwa watanzania katika maeneo mbalimbali hususani kwenye vyuo vya elimu ya juu pamoja na maeneo ya mikusanyiko.