Polisi katika jamhuri ya Congo mapemaJumanne walitumia gesi ya kutoa machozi kutawanya waandamanaji wanaopinga kura ya maoni inayolenga kumpa nafasi ya kubaki mdarakani rais Denis Sassou N’guesso.
Waandamanaji hao walichoma matairi na kufunga mitaa katika mji mkuu Brazzaville, huku huduma za simu na internet zikikatizwa kwenye eneo kubwa la mji huo. Congo itapiga kura jumapili kuhusu mapendekezo ya mageuzi yanayolenga kuondoa kipengele kilichoko kwenye katiba cha rais kuhudumu kwa mihula miwili na kuondoa umri uliowekwa kuhudumu hadi miaka 70 kwa rais.
Bila kufanya marekebisho hayo, Sassou N’guesso ambaye ameongoza Congo kwa miaka 31 hataweza kuwania wadhifa huo baada ya kipindi chake kuisha mwaka ujao. Alitangaza mipango wa kuitisha kura ya maoni mwezi uliopita, hatua iliyosababisha maelfu ya watu kuandamana katika mji wa Brazzaville.
Sassou N’guesso ailijipatia madaraka 1979 kwa njia ya mapinduzi ya kijeshi kisha akashindwa kwenye uchaguzi uliofanyika 1992. Alirejea madarakani tena 1997 baada ya mapigano yenye umwagikaji wa damu ya wenyewe kwa wenyewe, kisha baadaye akashinda kwenye uchaguzi wa 2002 na 2009 ambao ulisusiwa na vyama vingi vya siasa.
Sassou N’guesso ni mmoja wa viongozi wa afrika ambao wamesababisha mivutano kwa kujaribu kufanya marekebisho ya katiba ya kujiongeza muda wa kuhudumu.