Polisi huko Afrika Kusini wamefyatua risasi za mpira kwenye kundi la wafanyakazi wa umma ambao wako katika mgomo kudai ongezeko la malipo.
Maafisa walitawanya makundi ya watu katika maeneo mawili leo, katika kitongoji cha Soweto polisi waliondoa kundi la watu waliokuwa wanaziba barabara nje ya hospiatali, wakizuia wagonjwa kuingia.
Wakati huo huo Polisi walirusha risasi za mpira kwa walimu waliogoma huko Ormonde kitongoji cha Johannesburg wakati wakijaribu kuandamana kuelekea kwenye barabara kuu kuingia mjini.
Hakuna taarifa za watu kujeruhiwa kwa kiasi kikubwa katika eneo la hospitali. Hata hivyo huko Ormonde, polisi mmoja alionekana akivuja damu kichwani wakati waalimu waliporusha mawe na matofali kwa mapolisi.
Vyama vya wafanyakazi vinavyowakilisha waalimu milioni 1.3,wafanyakazi wa huduma na wafanyakazi wengine wa umma vilianza mgomo Jumatano vikidai nyongeza ya asilimia 8.6 na ongezeko la posho za nyumba.