Papa Francis Alhamisi aliwasihi maelfu ya vijana nchini Jamhuri ya Kidemokrasa ya Congo kufanya kazi kuelekea katika mustakbali mzuri na kujiepusha na rushwa katika nchi hiyo ya kikatoliki, ambayo imegubikwa na ghasia upande wa mashariki.
Papa huyo mwenye umri wa miaka 86 aliwasili katika uwanja wa Martyrs katika mji mkuu, Kinshasa, akiwa katika gari lake la kipapa, akiubariki umati uliokuwa na furaha kubwa, wakipiga kelele na kucheza.
Akihutubia uwanjani hapo, papa aliusihi umati kujenga hali njema ya siku za usoni kwa kanisa na nchi yao.
“Nyinyi ni lazima na mnawajibika kwa kanisa na nchi yenu. Nyinyi ni sehemu ya historia kubwa sana, ambayo inawataka kuchukua jukumu kama wajenzi wa ushirika, mabingwa wa udugu, wenye ndoto zenye tija kwa ajili ya dunia iliyoungana,” Papa Francis aliuambia umati.
Vijana wadogo walianza kumiminika wakati wa usiku kwenye uwanja huo wenye uwezo wa kupokea watu 80,000. Mkusanyiko wa Alhamisi ulikuwa na umati wa takriban watu 65,000, katika siku ya tatu ya ziara ya baba mtakatifu katika nchi idadi kubwa ya wakatoliki.
Kiasi cha asilimia 60 ya wakazi takriban milioni 100 katika taifa hilo la Afrika ya Kati wako katika umri wa chini ya miaka 20, kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa. Pamoja na mzozo, vijana wanakabiliwa na tatizo la ukosefu wa ajira.
Francis alikutana Jumatano na waathirika wa ukatili mbaya sana huko Mashariki mwa Congo ambako mapigano yanaendelea.
Aliwasikiliza akiwa amekaa kimya kupata ushuhuda wa moja kwa moja wa ukatili ambao baadhi yao wameupitia: kijana mmoja wa kiume alimuangalia baba yake akichinjwa; msichana mdogo ‘albakawa kama mnyama’ kwa miezi kadhaa; mtumwa wa zamani wa ngono ambaye alilazimisha kula nyama ya binadamu.
Catarina Legge, Muathirika wa Ghasia za Kivu Kaskazini: Nafsi yangu mimi mwenye baada ya kukutana na papa na sasa natulizana kwanza, na mie najua pamoja na Mungu vile tumeongea na papa mungu atasaidia. Maana kwa ujio wa papa nimesema mungu ambariki na kazi yake iendelee…"
Wacongo kutoka eneo la mashariki ambalo limegubikwa na ghasia walisafiri kwenda mji mkuu Kinshasa kumueleza papa juu ya ghasia za kutisha sana ambazo wamekumbana nazo kwa miaka kadhaa huku makundi ya waasi yakitaka kulikamata eneo hilo lenye utajiri mkubwa wa madini kupitia mashambulizi ambayo yamewalazimisha zaidi ya watu milioni 5 kukimbia makazi yao.
Muathirika wa Ghasia (hakutaka kutajwa jina: Hapo tulifurahia sisi tu tuko tunatafuta amani, hapa kwetu tunaishi katika hali ya vita, tumekimbia makazi yetu tuliporwa..."
Francis aliwaambia baada ya mkutano waathirika wa ukatili huko mashariki mwa Congo ‘ maumivu yenu ni maumivu yangu.’
Papa aliwaambia waliohudhuri mkutani wake “kwenu nyinyi, wakazi wa mashariki, nataka kusema: Mimi niko karibu na nyingi. Machozi yenu ni machozi yangu; maumivu yenu ni mauvimu yangu, kwa kila familia ambayo inaomboleza au imekoseshwa makazi kwasababu vijiji vimechomwa na uhalifu mwingine wa vita, kwa manusura wa ghasia za ngono na kwa kila mtoto na mtu mzima aliyejeruhiwa, nasema: niko pamoja nanyi; nataka niwaletee maliwazo ya mwenyenzi mungu.”
Papa yuko katika ziara ya siku sita barani Afrika, akiwa siku tatu huko Jamhuri ya Kidemokrasi ya congo na halafu atasafiri kwenda Sudan Kusini.
Chanzo cha habari hii ni Shirika la Habari la Reuters.