Majeshi yanayomuunga mkono Rais wa Ivory Coast, Alassane Ouattara yanawasaka wapiganaji ambao walimuunga mkono kiongozi wa zamani Laurent Gbagbo katika mji mkuu, Abidjan.
Wapiganaji washukiwa walichukuliwa kwenda kwenye hoteli ya Golf iliyopo Abidjan, ambayo ilihudumu kama makao makuu ya bwana Ouattara wakati wa miezi minne ya mapambano madaraka na bwana Gbagbo.
Kwingineko mjini Abidjan, kulikuwa na wizi na ufyatuaji wa silaha nzito leo Jumanne. Majeshi yanayomuunga mkono Ouattara yanajaribu kuwakusanya wanamgambo vijana wa bwana Gbagbo, hasa kiongozi wao Charles Ble Goude, ambaye alihudumu kama waziri wa vijana wa bwana Gbagbo.
Bwana Ouattara anatoa wito kwa wapiganaji wote kuweka chini silaha kufuatia kukamatwa kwa bwana Gbagbo. Umoja wa Mataifa inasema bwana Gbagbo na mke wake, Simone wameondolewa Abidjan, mahali ambapo walikuwa wakizuiliwa siku ya Jumatatu. Naibu msemaji wa Umoja wa Mataifa, Farhan Haq, anasema wawili hao wanaendelea kuwa chini ya ulinzi wa Umoja wa Mataifa kwenye sehemu isiyotajwa.
Bwana Gbagbo alikamatwa baada ya kukataa zaidi ya miezi minne kukubali kuwa alishindwa na bwana Ouattara katika uchaguzi wa Rais wa mwezi Novemba.
Akilihutubia taifa Jumatatu usiku, bwana Ouattara alitoa wito wa amani nchini humo ambapo miezi ya ghasia za baada ya uchaguzi imesababisha mamia ya watu n kuuwawa na kuwakosesha makazi hadi watu milioni moja. Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa ilisema leo, Jumanne kwamba kiasi cha watu 536 waliuwawa katika mapigano ya hivi karibuni huko magharibi mwa Ivory Coast.
Majeshi ya Ouattara yawasaka wafuasi wa Gbagbo
