Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Aprili 23, 2024 Local time: 14:13

Rais Obama atoa heshima kwa waathirika wa Sep 11, 2001


Rais Barack Obama(kati) akiwa na maafisa wa kituo kimoja cha polisi mjini New York ambacho maafisa wake walikuwa wa kwanza kufika katika tukio la Sep 11,2001
Rais Barack Obama(kati) akiwa na maafisa wa kituo kimoja cha polisi mjini New York ambacho maafisa wake walikuwa wa kwanza kufika katika tukio la Sep 11,2001

Rais wa Marekani Barack Obama amewaambia wafanyakazi wa idara ya zimamoto mjini New York hapa Marekani kwamba kifo cha Osama bin Laden kinapeleka ujumbe duniani kote kwamba Marekani haitasahau mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11 mwaka 2001.

Rais Obama yupo New York kutoa heshima kwa waathirika wa mashambulizi ya al-Qaida ya mwaka 2001. Ziara yake imekuja siku kadhaa baada ya majeshi ya Marekani kumuuwa kiongozi wa al-Qaida, Osama bin Laden.

Bwana Obama aliungana na meya wa zamani wa New York, Rudy Giuliani, alizungumza wakati alipokutana na wafanyakazi wa idara ya zimamoto ambao waliwapoteza wafanyakazi wake 15 katika mashambulizi hayo. Rais pia anatembelea kituo kimoja cha polisi katika eneo, ambacho maafisa wake walikuwa wa kwanza kufika katika eneo la tukio hapo Septemba 11.

Rais ameweka shada la maua kwenye majengo yaliyoharibiwa ya World Trade Centre. Anatarajiwa kukutana kwa faragha na ndugu wa wale waliouwawa katika mashambulizi ya ugaidi takribani muongo mmoja uliopita.

Msemaji wa rais, Jay Carney amesema jana Jumatano, kwamba bwana Obama anataka kukutana na familia hizo kuzungumza nao kufuatia kifo cha bin Laden.

Makamu Rais Joe Biden leo Alhamis ametoa heshima kwa waathirika wa Septemba 11 kwa kuweka shada la maua kwenye kumbukumbu ya Pentagon. Takribani watu 3,000 waliuwawa katika mashambulizi ya Septemba 11 mwaka 2001.

Kesho Ijumaa bwana Obama atasafiri kuelekea Kentucky kutoa heshima kwa wanajeshi kwenye kituo cha Fort Campbell ambao kilikisaidia kikosi maalum cha jeshi la majini katika shambulizi lao kwenye eneo la bin Laden siku ya Jumatatu karibu na kituo cha mafunzo ya jeshi, kwenye mji wa Abbottabad nchini Pakistan.

XS
SM
MD
LG