Rais Obama amesema kuwa ana uhakika kwamba Marekani itaweza kukabidhi juhudi za jeshi la kimataifa huko Libya kwa jumuiya ya kimataifa katika siku chache zijazo. Mwandishi wa VOA Dan Robinson anaripoti kuwa Rais alisema hayo huko El Salvador ambapo yeye na familia yake wanakamilisha ziara ya mataifa matatu ya Amerika ya kusini.
Ziara ya Rais huko El Salvador, baada ya kutembelea Chile na Brazil, imelenga katika kuimarisha uhusiano wa nchi hizi mbili na pia harakati za ukanda mzima kupambana na madawa ya kulevya.
Lakini akiwa Chile na Brazil, alikuwa amedhamiria zaidi katika maendeleo ya harakati za anga za kijeshi za majeshi ya Marekani kwa ushirikiano na nchi za Ulaya na Uarabuni, kutimiza azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la kulinda raia wa Libya kutokana na mashambulizi ya majeshi ya kiongozi wa nchi hiyo Moammar Gadhafi.
Bw. Obama amefanya mazungumzo na viongozi wa mataifa ya kigeni, wakiwemo Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy na Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron, na kabla ya hapo alizungumza na Waziri Mkuu, Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki.
Rais pia alijibu maswali kuhusu makabidhiano, ambayo yeye na maafisa wa utawala wake wamesisitiza kwamba watakabidhi kwa uangalizi wa kimataifa katika siku chache na sio wiki zijazo.
Katika mikutano yake wakati wa ziara ya Amerika ya Kusini, waandishi wa habari wamekuwa wakimuuliza Bw. Obama na maafisa wa Ikulu ya Marekani kuhusu hatua ambazo Marekani na washirika wake watachukua iwapo Kanali Gadhafi atagoma kuachia madaraka ama kuondoka Libya.
Rais amesema ni wazi kwamba Bw Gadhafi ataendelea kuwa tishio kwa watu wake ikiwa hataachia madaraka, ama kufanyika kwa mabadiliko muhimu, na kuongeza kuwa Marekani itaendelea kusaidia juhudi za kuwalinda raia wakati ikikabidhi harakati za kijeshi kwa washirika wake.
Mbali na maslahi ya kibinadamu, Rais ameeleza hali isiyo thabiti katika eneo kubwa la kaskazini mwa Afrika na Mashariki ya kati kama baadhi ya vitu anavyoona vikiwa na utata.
Aidha Rais Obama alionya juu ya uwezekano wa kuzuka machafuko zaidi nchini Libya na kuingia katika nchi za Misri na Tunisia ambapo anasema mabadiliko ya amani ya kisiasa yameanza.