HAVANA— Rais Barack Obama wa Marekani amesifu amesifu maendeleo yaliyopatikana baina ya Marekani na Cuba huku akikiri kwamba pande hizo mbili zinaendelea kuwa na "tofauti kubwa" katika maswala ya demokrasia na haki za binadamu.
Obama na Rais wa Cuba Raul Castro walifanya mkutano wa pamoja na waandishi wa habari baada ya mazungumzo yao mjini Havana kuhusu namna ya kurekebisha uhusiano wao.
Katika tukio la nadra, Castro alikubali kujibu maswali kutoka kwa waandishi baada ya viongozi hao wawili kutoa matamshi ya awali.
Castro alijibu kwa hasira baada ya kuulizwa swali kuhusu wafungwa wa kisiasa. Alitaka aonyeshwe orodha ya wafungwa hao, ikiwa ni katika msimamo wa Cuba kwamba haishikilii wafungwa wowote.
"Nipe orodha ya wafungwa hao sasa hivi na kama orodha ipo basi wataachiwa kabla usiku haujaisha," alisema Castro.
Siku ndani ya Havana
Obama na Castro walipeana mikono kabla ya kuingia katika mazungumzo yao katika jumba la mapinduzi - Revolutionary Palace - siku moja baada ya Obama kuwa Rais wa kwanza wa Marekani aliye madarakani kutembelea Cuba katika muda wa karibu miaka 90.
Mapema katika siku, Obama alihudhuria sherehe za kuweka shada la maua katika mnara wa shujaa wa uhuru wa Cuba Jose Marti katika Uwanja wa Mapinduzi mjini Havana.
Vikwazo vya Biashara
Vikwazo vya kibiashara vilivyowekwa na Marekani dhidi ya Cuba itabidi viondolewe na Bunge la Marekani linalodhibitiwa na Warepublican, lakini kuna kutokubaliana kuhusu sera ya Obama kubadili msimamo kutoka kuitenga Cuba na kwenda katika ushirikiano.
Ili kuweza kufanya sera mpya ya Marekani iendelee baada ya mwaka huu wa mwisho wa uongozi wa Obama, rais anahitaji uungwaji mkono kutoka pande zote mbili. Obama amekwenda Cuba na ujumbe mkubwa wa wabunge kutoka vyama vyote vya Democrat na Republican.