Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Aprili 17, 2024 Local time: 14:26

Hotuba ya Kuliaga Taifa: Obama asisitiza umoja na demokrasia


Rais Barack Obama akiwaaga wamarekani. Januari 2017.
Rais Barack Obama akiwaaga wamarekani. Januari 2017.

Rais Barack Obama amesema Jumanne Marekani hivi leo ina “ubora na nafasi yenye nguvu” kuliko alipochukua madaraka mwaka 2008, akionyesha jinsi alivyoweza kuboresha uchumi, kupitisha programu yake ya kihistoria ya afya na kuhalalisha ndoa za mashoga kuwa mafanikio ambayo watu wamarekani wameweka rekodi kupitia kauli mbiu yake ya mabadiliko.

Sehemu hiyo ya hotuba yake ya kuliaga taifa iliamsha hisia kubwa ya furaha na kushangiliwa kutoka kwa maelfu ya watu waliokusanyika huko Chicago kumsikiliza, kilomita chache kutoka katika eneo ambalo alitoa hotuba yake ya kukubali uongozi usiku alioshinda uchaguzi wake wa awamu ya kwanza kuingia ikulu ya White House.

Katika kipindi kisichozidi wiki mbili kabla rais mteule, Donald Trump kuapishwa, Obama alikuwa ameagiza timu yake kuandaa hotuba ambayo itaweza kuwa na athari kwa wamarekani wote, wakiwemo wale waliomchagua Trump.

Rais Barack Obama akitoa hotuba yake ya mwisho kama rais huko McCormick Place, Chicago, Jan. 10, 2017.
Rais Barack Obama akitoa hotuba yake ya mwisho kama rais huko McCormick Place, Chicago, Jan. 10, 2017.

Obama amesema katika hotuba yake ni juu ya wamarekani wote kuhakikisha kuwa serikali ina uwezo wa kutanzua changamoto nyingi zilizoko na ameahidi kukabidhi madaraka kwa uongozi mpya bila ya kuwepo vipingamizi vyovyote.

“Fahamuni kuwa demokrasia haihitaji kuwepo makubaliano,” alisema Obama. “Waasisi wetu walikuwa wanalumbana na kukubaliana, na walitegemea sisi tuwaige wao. Lakini walikuwa wanafahamu kuwa demokrasia inahitaji kuwa na hisia za mshikamano na fikra ya kwamba juu ya tofauti zote tulizokuwa nazo, bado sote sisi tuko katika taifa hili pamoja.

Obama ni mmarekani mweusi wa kwanza kuwa rais wa Marekani, na amesema kuwa baada ya kuchaguliwa kwake wengi walizungumza kile walichokiita ni Marekani mpya baada ya zama za ubaguzi. Lakini amesema bado suala la rangi ni “hai na lina nguvu katika kuwagawa watu” na kusisitiza kuwa kuna haja ya kuimarisha sheria zinazopinga ubaguzi.

Amehimiza makabila madogo kuunganisha harakati zao kupambana na changamoto zinazowakabili wakimbizi, wahamiaji, maskini katika vijiji na wale wamarekani waliobadili jinsia zao na kwa watu weupe kukubali kwamba sheria zilizokuwa zinawabagua wamarekani weusi zinaathari zilizodumu miaka mingi hata baada ya kupigwa marufuku.

Rais Barack Obama akifuta machozi alipokua anatoa hotuba yake ya mwisho huko McCormick Place, Chicago, Jan. 10, 2017.
Rais Barack Obama akifuta machozi alipokua anatoa hotuba yake ya mwisho huko McCormick Place, Chicago, Jan. 10, 2017.

“Kwa hivyo bila ya kujali eneo tulipo, lazima tujaribu kwa bidii; wote tunatakiwa kuanza na dhana ya kila mtu katika raia wenzetu anaipenda nchi hii kwa kiasi kile kile tunavyoipenda; wanathamini kufanya kazi kwa bidii na familia kama tunavyothamini sisi; na kuwa watoto wao wanashauku na matumaini na wanastahili kupendwa kama watoto wetu.”

Obama ameorodhesha mafanikio ya kiuchumi kama vile kupunguza idadi ya watu wasiokuwa na bima ya afya, kukuza uchumi na kupunguza idadi ya watu wasio na kazi. Lakini alisema hayo hayatoshi na kuwa bado tofauti katika vipato inaumiza misingi ya demokrasia nchini.

Wakati asilimia moja wamejilimbikizia kiwango kikubwa cha mali na kipato, familia nyingi katika miji midogo na vijiji kwenye kaunti, zimeachwa nyuma,” alisema Obama.

Obama amewaambia wanajeshi kwamba kule kuwa yeye alikuwa ni jemedari mkuu wao ilikuwa ni heshima kubwa maishani mwake, na kuelezea jinsi walivyoweza kupata mafanikio katika vita dhidi ya ugaidi, ikiwemo kuuwawa kwa aliyekuwa kiongozi wa al-Qaida Osama bin Laden na muungano ambao unafanya juhudi dhidi ya kundi la Islamic State nchini Syria na Iraq.

Rais pia amesema kuwa Marekani inawajibu wa kujilinda na njama zozote zitakazodhoofisha maadili yake katika hali ya vitisho, akielezea zaidi juhudi zake za kupiga marufuku utesaji, kufanya maboresho ya sheria za kuitahadharisha serikali na kufunga gereza la kijeshi huko Guantanamo Bay, Cuba.

“Hiyo ndio sababu napinga ubaguzi dhidi ya wamarekani waislamu,” alisema Obama, kauli ambayo inaweza kuwa iliamsha hisia kubwa kwa kushangiliwa usiku huo.

Mke wa rais, Michelle Obama akimpongeza mumewe Rais Obama baada ya hotba yake ya kuwaaga wamarekani.
Mke wa rais, Michelle Obama akimpongeza mumewe Rais Obama baada ya hotba yake ya kuwaaga wamarekani.

Amesema alikuwa na matuamini juu ya nchi hii kuliko wakati alipochukua urais. Lakini alihimiza pia kuwa watu washiriki kikamilifu katika harakati za kidemokrasia, akisema mfumo huo unategemea wamarekani “ kukubali jukumu la uraia bila ya kujali kule ambako misimamo ya kisiasa inaelemea.”

Wakati wa kampeni yake 2008, Obama alitumia kama moja ya kauli mbiu, “Change we can believe in,” ambayo ina maana ya mabadiliko tunayoweza kuyaamini.” Amerejea tena katika fikra hiyo katika hotuba yake ya mwisho Jumanne.

“Ninawataka muamini. Sio katika uwezo wangu wa kuleta mabadiliko, lakini katika uwezo wako mwenyewe,” alisema Obama.

XS
SM
MD
LG