Akizungumza baada ya kumaliza ziara ya siku mbili nchini Poland rais Obama alisema serikali ya Warsaw inaweza kuwa na jukumu la kipikee kuimarisha demokrasia barani Ulaya, Afrika Kaskazini na Mashariki ya Kati kutokana na historia yake yenyewe ya kuupinduwa utawala wa kikomunisti.
Kiongozi huyo wa Marekani akisimama na waziri mkuu wa Poland Donald Tusk, alisema Marekani na Poland zimekubaliana juu ya kuwekwa kwa kikosi cha anga cha Marekani nchini Poland kuanzia mwaka 2012 na kuanza mazowezi pamoja na jeshi la anga la Poland mapema mwaka 2013.
Mapema Jumamosi rais Obama alikutana na rais wa Poland Bronislwaw Komorowski na kupongeza kipindi cha vuguvugu la Solidarity cha mwaka 1980, ambacho kilifikisha kikomo ushawishi wa Urusi katika serikali ya Warsaw, kama wakati ambao, "wananchi wa kawaida wakisimama wima na kuchukua hatua za kipekee na kikishuja dhidi ya kitu ambacho hakikutarajiwa kitaweza kutendeka".