Rais wa Marekani Barack Obama anakuwa mwenyeji wa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu kwa mazungumzo ya Jumatatu wakati kiongozi huyo anafanya ziara yake ya kwanza mjini Washington tangu kundi la mataifa sita yenye nguvu duniani lilipotia saini mkataba wa nyuklia na Iran.
Bwana Netanyahu alikuwa mmojawapo wa wakosoaji wakuu wa mkataba wa nyuklia mwezi Julai, aliposema haitapunguza juhudi za Iran kufanya kazi zake za kuunda silaha za nyuklia na itaiweka Israel hatarini. Alielezea wasiwasi wake katika hotuba kwa bunge la Marekani linalodhibitiwa na wa-Republican hapo mwezi Machi wakati wa ziara yake ambayo hakukutana na bwana Obama.
Maafisa wa White House wanasema mkataba wa Iran utakua miongoni mwa masuala ya usalama wa kikanda ambayo Rais Obama na bwana Netanyahu watajadili hapo Jumatatu mjini Washington.