Rais Barack Obama ametangaza hali ya dharura kwa majimbo ya Florida na South Carolina nchini Marekani.
Maafisa wa jimbo la Florida pia wamewataka wakazi wa jimbo hilo kuondoka kutokana na kitisho cha kimbunga Mathew ambacho sasa kinatarajiwa kuingia jimboni humo huku maafisa wakiita kuwa ni jinamizi na ni kimbunga cha karne.
Kimbunga Mathew tayari kimesababisha vifo vya mamia ya watu kwenye visiwa vya Caribbean ikiwemo watu wasiopungua 283 huko Haiti. Hadi alhamis usiku kimbunga hicho kilipiga Grand Bahama Island na kinaelekea kaskazini-magharibi kwenye jimbo la Florida kikitarajiwa kufika mwanzoni mwa siku ya ijumaa.
Hiki ni kimbunga chenye nguvu kinachosafiri kilomita 210 kwa saa. Gavana wa Florida, Rick Scott amewatayarisha wanajeshi wa ulinzi wa taifa 3,500 ili kusaidia hali kwenye jimbo hilo. Wataalam wanasema maeneo ya jimbo hilo yatakuwa kwenye hali ya kudhibitiwa kwa wiki kadhaa baada ya kimbunga hicho kupiga.
Facebook Forum