Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 19, 2024 Local time: 20:24

Nyota ya Raila Odinga kuwa rais wa Kenya ‘imezima’


Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga akihutubia taifa baada ya tume ya uchaguzi IEBC kumtangaza Dr. William Ruto kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais Agosti 16, 2022. PICHA: Reuters
Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga akihutubia taifa baada ya tume ya uchaguzi IEBC kumtangaza Dr. William Ruto kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais Agosti 16, 2022. PICHA: Reuters

Ndoto ya Raila Odinga, mtoto wa makamu wa rais wa Kwanza wa Kenya Jaramogi Odinga, kuwa rais wa Jamhuri ya Kenya imeonekana kuzima kabisa hii leo, baada ya mahakama ya juu kuidhinisha ushindi wa Dr. William Ruto.

Hii imekuwa mara ya 5 kwa Raila Odinga, mwenye umri wa miaka 77, kugombea urais.

Odinga aligombea urais mara ya kwanza mwaka 1997 ambapo alimaliza katika nafasi ya tatu nyuma ya Daniel Arap Moi na Mwai Kibaki.

Alijiondoa kwenye kinyang’anyiro cha urais mwaka 2002 na kumuunga mkono Mwai Kibaki dhidi ya Uhuru Kenyatta.

Mwaka 2007, Raila Odinga aligombea urais dhidi ya Mwai Kibaki na akapata kura milioni 4.35 dhidi ya milioni 4.58 za Mwai Kibaki. Maandamano yalitokea, ghasia na mauaji ya maelfu ya watu. Kesi ilifunguliwa katika mahakama ya uhalifu wa kivita ICC. Aliunda serikali ya umoja wa taifa na Kibaki, na kuwa waziri mkuu. Serikali hiyo ilijulikani kama ‘nusu mkate’.

Mara ya tatu, Raila aligombea urais mwaka 2013 ambapo alishindwa na Uhuru Kenyatta. Alipata kura milioni 5.34. Kenyatta alipata kura milioni 6.17. Alipinga matokeo hayo mahakamani lakini ikatupiliwa mbali.

Mara ya nne alishindwa na Uhuru Kenyatta mwaka 2017. Kenyatta alipata kura milioni 7.7 huku Raila akipata kura milioni 6.3. Odinga alikataa matokeo hayo na kuelekea mahakamani ambapo matokeo yalitupiliwa mbali na kuagiza uchaguzi kurudiwa. Hata hivyo alisusia uchaguzi wa marudio uliofanyika na uhuru kupata kura milioni 7.48 huku Raila akipata kura 73,200. Alijiapisha kama rais. Uhuru Kenyatta alifanya mazungumzo na Raila na kukubaliana kushirikiana katika kuliunganisha taifa la Kenya.

Mara ya tano Raila Odinga kugombea urais ni mwaka huu 2022 ambapo ameshindwa na Dr. William Ruto. Aliasilisha kesi mahakamani kupinga ushindi wa Ruto wa kura milioni 7.1 dhidi ya zake alizopata milioni 6.9. Mahakama imetupilia mbali kesi hiyo kwa kukosekana Ushahidi na kusema tume ya uchaguzi IEBC iliandaa uchaguzi huo kwa njia ya wazi.

Wachambuzi wanasema itakuwa vigumu kwa Raila Odinga (77) kugombea urais miaka mitano ijayo kwa sababu ya umri. Wakati huo, atakuwa na umri wa miaka 82.

Viongozi walio karibu na Raila wamesema hawakubaliani na maamuzi ya mahakama

Mawakili wa Raila Odinga hata hivyo wamesema kwamba wanaheshimu lakini hawakubaliani na maamuzi ya mahakama kutupilia mbali keshi ya kupinga ushindi wa Dr. William Ruto.

Kiongozi wa mawakili wa Odinga, James Orengo, amesema kwamba “mahakama ilikosea katika uamuzi wake.”

Mgombea mwenza wa Odinga Martha Karua, naye ameandika ujumbe wa twiter akisema kwamba “mahakama ya juu imefanya uamuzi. Naheshimu uamuzi huo lakini sikubaliani nao.”

Katibu mkuu wa wafanyakazi COTU, ambaye pia ni mfuasi mkubwa wa Raila Odinga, Francis Atwoli amesema kwamba anakuabli maamuzi ya mahakama.

XS
SM
MD
LG