Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Aprili 20, 2024 Local time: 10:31

UN: Ukandamizaji unaotekelezwa na Nkurunziza umeongezeka


Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza
Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza

Ripoti ya jopo la tume ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa kuhusu Burundi  inaeleza kwamba serikali ya rais Pierre Nkurunziza imekuwa kandamizi zaidi. Tume hiyo ya watu watatu inasema hali hiyo si ishara nzuri wakati nchi hiyo ikielekea kwa uchaguzi mkuu mwaka ujao.

Kupitia ripoti hiyo, iliyowasilishwa kwa baraza la Umoja wa Mataifa la haki za binadamu wiki hii mjini Geneva, jopo hilo limeelezea kusikitishwa na hatua ya Burundi ya hivi karibuni kufungwa ofisi ya UN ya haki za binadamu baada ya kuwepo nchini humo kwa takriban miaka 23.

Tume hiyo ya uchunguzi ni taasisi pekee ya kimataifa ambayo inafuatilia hali ya haki za binadamu nchini Burundi.

Ripoti hiyo inaelezea kwamba Burundi imeziambia taasisi zote zisizo za kiserikali ambazo ni za kigeni kujiandikisha tena na kuwasilisha orodha ya wafanyakazi wake na pia kutaja ukabila wao.

Hili limefanyika ili kuona kama wanatekeleza mfumo wa mgao mpya uliowekwa kutaka asilimia 60 wawe wa kabila la Hutu na asilimia 40 wawe Watutsi na pia kuangalia kama wanatekeleza kiwango cha chini cha kuwa na wanawake asilimia 30.

Mjumbe mmoja wa tume hiyo, Francoise Hampson, amesema baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali yametangaza kuwa yataondoka nchini badala ya kutekeleza masharti hayo ambayo wanasema ni kinyume na thamini zao.

"Kuendelea kusinyaa kwa mwanya wa kidemokrasia pia kunaathiri mashirika yasiyo ya kiserikali ya ndani ya nchi, watetezi wa haki za binadamu, na vyombo huru vya habari nchini Burundi. Hili linatia wasi wasi zaidi hasa ukizingatia kuwa uchaguzi mkuu utafanyika mwaka 2020," alisema Hampson.

Wajumbe wa tume hiyo wanasema mzozo wa kisiasa ambao ulizuka nchini Burundi mwaka 2015 wakati Nkurunziza alipotangaza kuwania awamu ya tatu ya uongozi haujasuluhishwa bado.

Wanakhofia hili litakuwa na athari kubwa sana mwaka 2020 na kusema wamepata habari kwamba wanachama wa upinzani wanatishiwa, kunyanyaswa, kukamatwa au hata kupotea kabisa.

Balozi wa Burundi kwenye Umoja wa Mataifa huko Geneva, Renovat Tabu, aliwashutumu wanachama wa tume hiyo akiwaita mamluki ambao ni nyenzo ya upinzani nchini humo.

Alipuuza ripoti yao kuwa imejaa uongo, kashfa, matusi na taarifa za kisiasa.

Mwisho wa malumbano, rais wa baraza la haki za binadamu alimkemea balozi, na kumtaka asite kufanya mashambulizi binafsi na azungumze kwa heshima.

-Imeandikwa na Lisa Schlein, mwandishi wa VOA mjini Geneva, Uswizi.

XS
SM
MD
LG