Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Mei 28, 2023 Local time: 22:07

Waasi wa FNL washutumiwa kuuwa Burundi


Miili ya waathirika katika shambulizi la kwenye baa Jumapili usiku huko Gatumba nchini Burundi. Septemba 19, 2011

Rais Nkurunzinza wa Burundi ameapa kuwasaka watu waliofanya mashambulizi nchini kwake na kusababisha vifo kwa raia

Rais wa Burundi ameapa kuwasaka watu wenye silaha ambao walishambulia baa moja karibu na mpaka na Congo Jumapili usiku, na kuuwa watu wasiopungua 36.

Rais Pierre Nkurunzinza alisema Jumatatu kwamba washambuliaji wanaaminika wamevuka mpaka kutoka Congo, japokuwa maafisa wa usalama bado hawajaelezea nani alihusika kwenye mauaji hayo. Mashahidi wanasema waasi hao waliingia katika baa hiyo jana usiku na kuamuru watu kulala chini na kuanza kuwafyatulia risasi.
Tukio hilo limetokea huko Gatumba, kiasi cha kilomita 15 magharibi ya mji mkuu Bujumbura na kiasi cha kilomita tano kutoka mashariki ya Congo. Maafisa wa usalama wanasema watu 23 walikufa hapo hapo katika tukio na wengine 13 walikufa baada ya kufikishwa hospitali.

Baada ya kulitembelea eneo Rais Nkurunzinza alitangaza siku tatu za maombolezo na aliahidi Burundi italitatua suala hili katika kipindi cha mwezi mmoja.

Mwandishi mmoja wa habari katika eneo ameiambia Sauti ya Amerika kwamba Rais alisema kwamba huenda akaomba msaada wa kimataifa katika kutatua suala la uhalifu kama ikibidi. Anaripoti kuwa Rais pia alisema washambuliaji hivi sasa walikuwa wamejificha nje ya nchi.

Katika ripoti ya shirika la habari la Associated Press, msemaji wa jeshi la Congo, Sylvain Ekenge alisema kwamba alishangazwa na madai ya washambuliaji kutoka nchini kwake. Ekenge alisema inaonekana kuwa walikuwa sehemu ya jeshi la uasi la mwaka jana la nchini Burundi la Forces for National Liberation-FNL.

Burundi imekuwa nchi ya amani tangu kundi la FNL walipoweka silaha chini mwaka 2009 baada ya miaka 20 ya uasi. Lakini mashambulizi yameongeza khofu ya kurejea kwa mgogoro. Serikali inalaumu idadi kadhaa ya mashambulizi ya awali mwaka huu kufanywa na magenge ya wahalifu wenye silaha.

Katika taarifa ya Jumatatu, katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon alilaani ghasia hizo akisema hazina msingi na alivitaka vyama vyote nchini Burundi kutumia busara kutatua tatizo hili.

XS
SM
MD
LG