Shambulio hilo lilifanyika saa chache baada ya watu wenye silaha kufyatulia risasi msafara wa Rais Muhammadu Buhari katika jimbo la Katsina alikozaliwa.
Shambulio dhidi ya gereza hilo la Abuja ni tukio la hivi karibuni katika msururu wa mashambulizi mabaya yanayotekelezwa na makundi yenye silaha nchini Nigeria.
Watu wenye silaha nzito walivamia jela hilo Jumanne usiku, kwa kufyatua risasi na kulipua vilipuzi.
Maafisa wanasema askari mmoja wa kulinda gereza aliuawa na wafungwa 600 waliachiwa huru na washambuliaji kabla ya kufurushwa na maafisa wa usalama.
Kulikuwa ulinzi mkali kwenye jela hilo jana Jumatano huku maafisa wakisema wameanza msako wa wafungwa waliotoroka. Maafisa wanasema watoro 300 wamekamatwa tena.
Jumatano, ndugu wa wafungwa walikusanyika kwenye uwanja wa gereza wakitarajia taarifa mpya kutoka kwa mamlaka ya gereza.
Hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulio hilo la Jumanne, lakini maafisa wanalishuku kundi la kigaidi la Boko Haram.